Kiasi cha asilimia 2 ya mimba
zote hutungwa nje ya mji wa uzazi. Hali hii hujuilikana kama
ectopic pregnancy kwa kiingereza au extrauterine pregnancy kwa kitaalamu. Mara
nyingi mimba zinazotunga nje ya kizazi huwa haziwezi kukua mpaka mwisho wa
ujauzito, huweza kuleta hatari kwa afya ya mama hasa pale inapopasuka na
kuvujisha damu tumboni mwa mama.
Kama
uliwahi kupata mimba nje ya uzazi kabla ya hii, maambukizi kwenye mirija ya
uzazi, upasuaji kwenye mirija ya uzazi au historia ya ugumba huongeza uwezekano
wa tatizo kujirudia au kuwa mgumba.
Namna Mimba Za Nje ya Kizazi Zinavyotokea
Kwa kawaida mbegu ya kiume na yai
la kike hukutana katika mirija ya uzazi (Fallopian tubes) na mimba hutungwa.
Kiinitete husafri polepole kwenda kwenye mji wa uzazi ambako hujipandikiza
kwenye ukuta wa uzazi na mimba huanza kukua. Katika ugonjwa huu wa mimba kuwa
nje ya kizazi (ectopic pregnancy) mbegu ya kiume na yai huungana kutengeneza
kiinitete. Badala ya kupandikizwa kwenye tumbo la uzazi, kiinitete huenda
kujipandikiza sehemu nyingine tofauti na mji wa uzazi. Kinaweza kujipandikiza
kwenye mirija ya uzazi, ovari, kwenye shingo ya uzazi na ndani ya tumbo
(abdominal cavity). Mimba nyingi za nje ya kizazi hujipandikiza kwenye mirija
ya uzazi ambapo huwa na hatari ya kupasuka kadri mimba inavyokua.
Mara chache sana mimba zinazotunga nje ya kizazi huweza
kukua mpaka mwisho, nyingi huishia kupasuka na kuondolewa kwa upasuaji.
Sababu Hatarishi za Mimba Kutunga Nje ya Kizazi
Zifuatazo ni baadhi ya sababu
zinazochangia kutokea kwa mimba za nje ya kizazi.
- Umri wa zaidi ya miaka 40 kwa mwanamke
- Uvutaji sigara
- Matumizi ya vijiti vya mji wa uzazi (intrauterine devices)
- Kutoa mimba zaidi ya 3
- Upasuaji wa mirija ya maji ya uzazi
- Ugonjwa wa PID
- Matumizi ya dawa ya diethylstilbestrol (DES)
- Teknolojia saidizi za uzazi (assisted reproduction)
- Ingawa wakati mwingine zinazoweza kutokea bila sababu maalum kujulikana.
Dalili
Kufuatia wiki kadhaa baada ya
kukosa siku zako za hedhi, unaweza kuanza kupata maumivu ya tumbo chini ya
kitovu au kiuno, ambayo yanaweza kuwa upande mmoja. Maumivu yanaweza kuja na
kuacha, kuwa makali sana
kiasi cha kushindwa kuvumilia.
Hali hii inaambatana na kutokwa
damu ukeni, mara nyingi ikitoka kidogo kidogo. Inaweza kuwa nyepesi au nzito
nyeusi.
Wakati mwingine unaweza usipate
dalili zozote, tatizo likagunduliwa wakati wa kipimo cha ultrasound. Kuna
baadhi ya watu wanaweza wasipate dalili zozote na mimba kukua nje ya kizazi
mpaka wakati wa kujifungua kukaribia.
Vipimo
Tatizo hili hugunduliwa kwa
kipimo cha ujauzito (kwa mkojo au damu) kuthibisha kama
mtu ana mimba na kisha ultrasound ya tumbo ili kuona mimba ilipo.
Kipimo cha mimba. Kipimo cha
mimba cha mkojo (urinary pregnancy test) au cha mimba cha damu (serum HCG)
hufanyika kuthibitisha uwepo wa mimba.
Ultrasound ya tumbo. Hii
hufanyika kuonesha mimba ilipo. Wakati mwingine kwa wiki za mwanzoni (chini ya
wiki 5) mimba iliyo nje ya kizazi inaweza kuwa ngumu kuiona kwenye ultrasound. Kama ipo nje ya kizazi au imepasuka itaonekana kwa kipimo
hiki.
Matibabu
Matibabu ya mimba nje ya kizazi
yanaweza kuwa ya dawa peke yake au kwa njia ya upasuaji. Matibabu ya dawa
huanzishwa pale ambapo mimba ni ndogo na viwango vya hcg kwenye dami si vikubwa
sana . Unaweza
ukapewa dawa moja au mchanganyiko na ukawekwa kwenye ufuatiliaji wa karibu
mpaka utakapopona.
Matibabu ya upasuaji hufanywa
pale mimba inapopasuka, kuwa kubwa au mara chache imekomaa karibu na
kujifungua. Upasuaji huusisha kuuondoa mimba iliyo nje ya uzazi, kama mirija imehusika basi kukata sehemu iliyoharibika na
kuunganisha tena. Wakati mwingine mirija huondolewa moja kwa moja. Kwa mtoto
ambaye ameshakomaa, tumbo hupasuliwa na mtoto kuondolewa.
Kupata Ujauzito Tena
Kwa wanawake wanaotarajia kupata
tena ujauzito baada ya matibabu ya mimba kutunga nje ya uzazi, huweza kupata
ujauzito wa kawaida. Ila kuna mambo matatu;
- kupata mimba ya kawaida,
- mimba kutunga tena nje ya kizazi au
- kupata ugumba.
Unaweza kupata ujauzito wa
kawaida baada ya mimba kutunga nje ya kizazi. Zaidi ya asilimia 80 ya wanawake
huenda kupata ujauzito wa kawaida baada ya kupona.