Kambale (Ietalurus Punetaus), ni
aiana ya samaki ambao wana majina mengi kulingana na eneo na jamii husika.
Samaki hawa unaweza kusikia wakitajwa kwa majina mengine kama
vile, kambale channel, koleo, samaki kidevu n.k.
Kwa
maelezo zaidi juu ya ufugaji wa samaki, unaweza kuwasiliana na mtaalamu wa
samaki Bw. Musa Said Ngematwa kwa simu +255718 986 328
Asili ya samaki hawa ni Amerika
ya Kaskazini. Samaki hawa hukua kwa haraka sana , na kuwa na uzito mkubwa. Aina hii ya
samaki hupendwa na watu wengi kwa kuwa nyama yake ina ladha nzuri na ni laini sana .
Samaki hawa huzaliana vizuri
zaidi wanapokuwa mtoni au sehemu ambayo wanapata tope. Mfugaji anapokusudia
kufuga aina hii ya samaki kibiashara, ni lazima kusakafia bwawa ili kuepuka
uharibifu unaoweza kusababishwa na samaki hawa.
Umbile
Samaki aina ya kambale wana umbo
refu, mpana kuanzia shingoni, ingawa kichwa ni kidogo, na upande wa mkia ni
mwembamba. Samaki hawa wana rangi ya kijivu na wengine nyeusi.
Kulisha
Unaweza kulisha kambale kwa
kutumia unga wa samaki, maharagwe yaliyosagwa, mahindi, mchele pumba, ngano na
bidhaa nyingine. Unaweza kujenga mfumo ambao utawawezesha samaki hawa kupata
aina mbalimbali za wadudu, pamoja na majani, ili kusaidia wapate mlo kamili.
Ukuaji na uvunaji
Aina hii ya samaki, wakitunzwa
vizuri, wanaweza kukua kwa haraka na kuwa na uzito mzuri unaoweza kumpatia
mfugaji faida nzuri. Unaweza kuanza kuvuna kambale baada ya miezi sita tangu
walipopandikizwa kwenye bwawa.
Fikiria soko la samaki kabla ya kuanza kuzalisha
Wafugaji walio wengi, wamekuwa
wakianzisha miradi ya ufugaji wa samaki kwa kufuata mkumbo bila kutambua kwanza
soko watakalozalishia samaki hao. Jambo hili huwafanya wafugaji kuwa na kipato
kidogo tofauti na nguvu waliyotumia kuzalisha.
Inapofikia wakati wa kuvuna
samaki, kiasi kikubwa huuzwa papo hapo bila kufika kwenye soko halisi, jambo
linalosababisha kipato kuwa duni. Ni vyema mfugaji akawa na soko maalumu ambalo
atazalishia. Unaweza kuzalisha kwa ajili ya shule, hospitali, vyuo, au taasisi
yoyote. Halikadhalika jamii inayokuzunguka na taasisi nyinginezo.
Ni vizuri kuzingatia yafuatayo kabla ya kuanza uzalishaji wa samaki
• Fahamu ni aina gani ya samaki
inayopendwa zaidi katika eneo ulipo.
• Samaki wanaopendwa wanatakiwa
wawe na ukubwa gani.
• Kiasi cha samaki
kinachohitajika katika soko ulipo.
• Ni kipindi gani ni kizuri kwa
uvunaji wa samaki.
• Ni wakati gani mzuri wa kuuza
samaki.
• Je, katika eneo lako kuna
mfugaji mwingine anaezalisha samaki kwa ajili ya soko hilo ?.
• Bei ya aina ya samaki
unaozalisha ikoje?
Wasikilize wateja
Wakati wote mfugaji anapouza
samaki, ni lazima kusikiliza kwa umakini, wateja wako wanasemaje.
• Je, wanapendelea samaki
unaouza.
• Je, samaki wako ni wadogo sana au ni wakubwa sana .
• Wakija kununua wananunua kwa
kiasi gani, kikubwa au kidogo.
• Je, wanapendelea uzalishe
zaidi?
• Je, kuna wafanyabiashara
wanataka uzalishe zaidi ili nao wanunue.
• Wanataka samaki wawe kwenye
ubora gani.
• Wanaridhika na bei unayowauzia.
Fuata haya kwa ufanisi wa soko la samaki
• Hakikisha samaki wako katika
hali ya usafi na vyombo salama unapovua tayari kwa kupeleka sokoni.
• Samaki ni bidhaa inayoharibika
kwa haraka, hivyo hakikisha unawapeleka sokoni mara tu baada ya kuwavua.
• Hakikisha gharama za usafiri,
utunzaji na uhifadhi, zinalipwa kutokana na bei ya soko.
• Kumbuka gharama za uhifadhi wa
bidhaa inayoharibika haraka kama samaki ni
kubwa, hivyo vua kwa awamu kulingana na mahitaji.
• Unaweza kuongeza thamani ya
samaki kwa kufanya mambo ya msingi yanayohitajika kwenye uandaaji wa samaki, kama vile kuparua na kutumbua.
• Unaweza kuwasafisha, na pia
kuwakaanga kulingana na soko husika.
Kwa kuzingatia mambo hayo
machache, mfugaji anaweza kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuwekeza kwenye mradi
wa ufugaji wa samaki. Pia ni muhimu kuzingatia mahitaji muhimu ya ufugaji wa
samaki, ili kuepuka gharama zisizo za lazima.
Tengeneza chakula cha samaki mwenyewe
PAGE 7Mfugaji anaweza kupunguza
gaharama za kununua chakula kwa ajili ya samaki, kwa kutengeneza chakula
mwenyewe kwa kutumia malighafi ulizo nazo katika eneo lako. Tumia resheni
rahisi ambayo itakupatia chakula cha kutosha na kwa gharama nafuu.
Mahitaji
• Pumba ya mahindi sadolini 1.
• Pumba ya ngano au mpunga
sadolini 1.
• Dagaa sadolini 1.
• Kilo moja ya soya.
• Robo kilo ya mashudu ya pamba
au alizeti.
Namna ya kuandaa
• Changanya malighafi hizo kwa
pamoja.
• Saga hadi zilainike.
• Kanda kama vile unga wa
kutengenezea chapati.
• Weka kwenye mashine ya kusaga
nyama au kutengenezea tambi.
• Anika kwenye jua la wastani.
• Baada ya kukauka, vunja vunja
kwenye vipande vidogo vidogo hasa kwa kuzingatia umri wa samaki unaokusudia
kuwalisha.
• Tumia lishe hiyo kwa samaki
mara tatu kwa siku.