F SOYA: MATUMIZI, FAIDA NA HASARA ZAKE | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

SOYA: MATUMIZI, FAIDA NA HASARA ZAKE

Soya ni mmea jamii ya mikunde ambao ni maarufu sana kutokana na kuwa chanzo kizuri cha protini katika lishe ya binadamu. Soya ina protini nyingi na hutumika sana na watu wasiokula nyama kama chanzo cha protini. Zao hili hulimwa sana sehemu mbalimbali duniani. Soya baada ya kuvunwa huweza kutengenezwa bidhaa za soya kama maziwa ya soya, nyama ya soya (tofu), miso, tempeh.

Soya ina protini ambayo ina ubora mzuri kama wa protini za wanyama. Soya ni kati ya makundi ya chakula mabayo yanafanyiwa utafiti sana juu ya faida na madhara ya matumizi yake kutokana na kutumika sana katika lishe. Maziwa mengi ya watoto sasa yanatumia soya kama mojawapo ya vyanzo vya protini.

Virutubisho
Soya ina virutubisho vingi hasa protini kwa wingi, madini ya Kalsiamu, Vitamini B, Omega -6 na kambakamba (fiber).

Soya zina kampaundi ziitwazo phytoestrogens, ambazo hupatikana katika mimea. Kuna iana mbalimbali za phytoestrogens, lakini zinazopatikana kwa wingi kwenye soya ni isoflavones. Isoflavone zinadhaniwa kuleta faida nyingi kiafya kwa watumiaji wa soya na inafanana kwa kiasi na homoni za kundi la estrojeni.

Matumizi
Soya hutumika kutengeneza vyakula vya aina nyingi. Unaweza ukatumia soya kama;

  • Maziwa ya soya
  • Kinywaji cha soya (kama chai)
  • Mboga ya kupika kama edamame
  • Nyama za soya
  • Virutubisho vya soya (soy supplements)
  • Soya ni lazima ipikwe vizuri, Ikiwa mbichi soya ni sumu na inaweza kuleta madhara kwa afya yako.Utumiaji wa soya kwa wingi kwenye mlo wako itakusaidia kupata protini ya hali ya juu, madini kama kalsiamu. Unaweza kutumia bidhaa mbalimbali za soya kama mbadala wa protini zinazotokana na wanyama.


FAIDA ZA SOYA KIAFYA
Soya ni kati ya vyakula vinavyoaminika kuwa na faida nyingi kiafya inapotumika katika mlo wa mtu. Tafiti nyingi zinaendelea kufanyika kuhusu faida za soya, na nyingi zikionesha faida zake ingawa baadhi hazijaweza kuthibitisha faida zinazoaminika kutokana na soya.

Soya Inasaidia Kupunguza Ukali wa Dalili za Hedhi Kukoma (Menopause)
Dalili kama kuona joto sana, hasa usoni na kutokwa na jasho zinaweza kupunguzwa kwa kiasi na utumiaji wa vyakula vyenye soya. Pale hedhi za mwanamke zinapoanza kukoma, uzalishwaji wa homoni za estrojeni hupungua na hivyo kupata dalili za kuhisi kama joto kali usoni na kutokwa jasho. Matumizi ya soya yanasaidia kupunguza dalili hizi kwa phytoestrogens kufanya kazi kama estrojeni mwilini mwa mwanamke.

Kupunguza Ukali wa Homoni za Estrojeni Mwilini
Phytoestrogens ni kampaundi zinazofanana na homoni za estrojeni, hivyo husaidia kupunguza ukali wa estrojeni pale inapokuwa nyingi mwilini kama kwenye hali kama PMS (kabla ya kuingia hedhi) na endometriosis.

Kupunguza Lehemu Mwilini
Soya inasaidia kupunguza lehemu (cholesterol) mwilini kwa kupunguza unyonywaji wa lehemu kwenye utumbo wa chakula. Soya zina phytosterols ambazo zinafanana na lehemu,lakini hazina madhara ya lehemu. Phytosterols huzuia kunywa kwa lehemu na hivyo kupunguza kiasi cha lehemu mwilini.

Hupunguza Hatari ya Saratani ya Matiti Kwa Wanawake
Kuna baadhi ya tafiti zinaashiria wanawake wanaotumia soya kwa wingi katika mlo wao huwa na hatari ndogo ya kupata saratani ya matiti. Hii inadhaniwa ni kutokana na kampaundi za isoflavones. Hata hivyo bado hakujakuwa na ushahidi wa kutosha kitafiti kuthibitisha hilo.

Ingawa kwa kiasi kikubwa soya inadhaniwa kusaidia afya ya moyo na mifupa kwa wanawake, bado tafiti hazijaweza kuthibitisha hilo kwa uhakika.

MADHARA NA TAHADHARI
Matumizi ya soya yanaweza kuleta madhara kwa watumiaji;

  • Soya zinaweza kuleta allergy kwa baadhi ya watumiaji.
  • Soya ambazo mbichi au zimepikwa zina kampaundi ziitwazo goitrogens ambazo zinaweza kuingilia ufanyaji kazi wa tezi ya shingo (thyroid gland).
  • Watu wenye mawe ya figo (kidney stones) yenye oxalate hawatakiwi kula soya kwa wingi kwani zina madini ya oxalate, na hiyo kuweza kuchangia mawe haya.
  • Wanawake wenye saratani ya matiti (oestrogen-sensitive breast tumours ) wanatakiwa kutumia soya na bidhaa zake kwa kiasi kidogo.
  • Phytoestrogens ikijumuisha na isoflavones zimekuwa zikihofiwa kwamba zinaweza kuleta madhara kwenye ukuaji na maendeleo ya jinsia, kinga na mfumo wa uzazi kwa watoto wachanga wanaotumia maziwa yenye soya. Ingawa baadhi ya tafiti kwa wanyama zimeonesha hivyo, bado hakuna ushahidi unaonesha madhara kwa binadamu.


Soya inaweza kuwa na faida kwako kiafya, na kwa mwingine isimletee faida kubwa sana. Kitu muhimu ni kujitahidi kuchanganya aina mbalimbali za vyakula. Hakuna chakula kimoja chenye virutubisho vyote mwili unavyohitaji. Kama unapata madhara ukitumia soya, basi acha na tafuta vyanzo vingine vya protini ambavyo havitaleta madhara kwako.