Bila shaka kula chakula chenye virutubisho sahihi ni jukumu la lazima la binadamu kama anahitaji kuwa na afya njema. Dunia ina vyakula vya asili ambavyo ndani yake kuna virutubisho muhimu vinavyosaidia mwili kupambana na magonjwa na pia kuimarisha afya. Vyakula hivyo si vingine bali ni vile vya kijani ambavyo vina uwezo mkubwa zaidi katika kuponya magonjwa na kusaidia pia kukarabati, kujenga mwili na kuimarisha siha. Ngozi nayo ni sehemu muhimu ya mwili ambayo ina jukumu kubwa la kuukinga na kuufunika mwili na viungo mbalimbali na afya yake ni jambo la kuzingatiwa. Jenetiki na muundo wa maisha wa watu vina taathira kubwa katika afya ya ngozi, ambapo pia aina za vyakula tunavyopendelea kula vinaweza kuchangia katika muonekano wa ngozi zetu na kusaidia kupambana na matatizo ya ngozi, kupunguza mikunjano ya uso na suala zima la afya na muonekano wa ngozi.
Huenda wote tunapenda kuonekana warembo na vijana, lakini kutofahamu njia sahihi za kudumisha urembo wa mwili na ngozi huenda kukawafanya baadhi ya wasifikie lengo hilo na hata kujiletea madhara makubwa yasiyotibika hapo baadae. Pia inawezekana tukatumia hela nyingi na muda mwingi katika kuhakikisha ngozi inakuwa nyororo, nzuri na ya kuvutia lakini pengine ukawa hufahamu kuwa kuna aina za vyakula vinavyosaidia katika kutunza ngozi yako na tena bila gharama kubwa.
Bi Samatha Heller mtaalamu wa lishe katika Chuo Kikuu cha Tiba cha New York City anasema kuwa, kila tunachokula kinakuwa sehemu ya mwili wetu ikiwa ni pamoja na sehemu ya nje na kwamba, kila tunavyokula vyakula bora ndivyo ngozi zinavyoonekana vizuri. Naye Elein Linker mtaalamu wa biokemikali na mwasisi wa kituo cha kutunza ngozi cha DDF anasema kwamba, matatizo mengi ya ngozi kama vile chunusi ya aczema yanaweza kuwa yanahusiana na liche. Kwa ajili hiyo tunashauriwa kuwa, kama ambavyo tunajitahidi kufuata kanuni za afya ili kuufanya mwili uwe na afya nzuri kwa kula chakula bora, kufanya mazoezi mara kwa mara, kupumzika kwa muda mrefu, vivyo hivyo ngozi nayo inatakiwa kutunzwa vyema kupitia lishe.
Vifuatavyo ni vyakula vinavyoweza kusaidia kuimarisha afya ya ngozi:-
Chakula cha kwanza chenye uwezo wa kuimarisha siha ya ngozi ni asali. Asali ambayo hutengenezwa na nyuki kwa viambato asilia ni chakula muhimu kwa ajili ya kuimarisha afya ya ngozi na pia afya ya binadamu. Chochote kile ambacho ni kizuri kwa afya yako ni nzuri kwa ngozi pia, hivyo ngozi yenye afya inatakiwa kuhifadhi unyevunyevu ili kuzuia kukauka na kupasuka.
Hii ndio sababu kubwa ya kutumia mafuta ili kuifanya ngozi iwe na unyevu. Asali husaidia kutunza na kuhifadhi unyevu kwenye ngozi na ina kiwango kikubwa cha sukari na asidi ambazo huzuia vijidudu wanaozaliana kwenye ngozi. Tunashauriwa kuwa, ili kuweza kulinda ngozi, paka asali wakati wa kuoga, acha kwa muda kisha ioshe. Kufanya hivyo kunaweza kuinawirisha ngozi. Vyakula vya baharini kwa ujumla ni vizuri kwa afya, lakini faida haishii kwenye afya ya mwili tu, bali inasaidia hata kwenye ngozi.
Vyakula vingi vya baharini vina kiwango kikubwa cha Zinc na Omega 3 ambazo ni muhimu kwa siha ya ngozi. Faida za Omega 3 ni pamoja na kuondoa kukakamaa au ukavu wa ngozi, kupunguza kuvimba na kukunjamana kwa ngozi na husaidia mzunguko mzuri wa damu mwilini hivyo kuboresha ngozi. Damu inapozunguka vyema mwilini afya ya ngozi hayo huimarika. Hii ni katika hali ambayo Zinc husaidia kuondoa chunusi na harara katika ngozi kwa kuyeyusha homoni ya testosterone. Pia husaidia kuzalishwa seli au chembe hai za mwili na kuondoa chembe zilizokufa huku ikiifanya ngozi ing'ae na kuwa na mvuto.
Chakula kingine muhimu kwa ajili ya kuimarisha siha ya ngozi ni mayai. Nadhani si ajabu kusema kuwa yai ni kirutubisho muhimu kwa afya kwani lina virutubisho muhimu sana kwa afya ya ngozi. Kiini cha yai kina vitamini A na B huku sehemu yenye ute ikiwa na protini nyingi ambayo ni muhimu pia kwa ngozi . Mada ya Tretinoin inayopatikana kwenye Vitamin A husaidia kuondoa chunusi na mikunjo ya ngozi. Mada nyingine ya Biotin inayopatikana kwenye Vitamin B ni muhimu kwa afya ya ngozi na kucha na protini inayopatikana kwenye ute wa yai ni muhimu katika kuifanya ngozi iwe nyororo na yenye kung'aa na pia husaidia ngozi kujilinda vizuri na mionzi ya jua.
Mpenzi msikilizaji matunda yenye vitamini C kama vile chungwa, limao na mengineyo ni muhimu pia katika kuimarisha afya ya ngozi, kwa sababu husaida kutengeneza collagen, ambayo ni aina ya protini inayotengeneza ngozi. Vitamini C inasaidia kuondoa uvimbe na mikunjo ya ngozi na hivyo kuilinda ngozi isizeeke mapema. Chakula kingine muhimu kwa siha ya ngozi ni shayiri. Chakula hiki kina virutubisho muhimu vya kusaidia ngozi na ni kama mafuta yanayolainisha ngozi.
Katika shayiri kuna virutubisho tofauti kama vile polysaccharides ambayo huzuia kupasuka kwa ngozi kutokana na ukavu. Saponins, inayosaidia kusafisha ngozi na kuzuia fungus na vijidudu, na Polyphenols inayozuia uvimbe wa ngozi. Pia wanga huhifadhi unyevunyevu kwenye ngozi. Mboga za majani pia ni muhimu kwa afya ya ngozi kama tujuavyo zimesheheni vitamin na virutubisho vya aina mbalimbali vyenye faida kubwa kwa ngozi na mwili kwa ujumla. Kama unataka uwe na ngozi nyororo unapaswa kutosahau kula mboga kama vile broccoli , karoti na maboga ambazo zina vitamini A na Zinc.
Vitamin A ni muhimu kwenye ngozi kwa sababu husaidia ngozi kuzalisha seli mpya na kuondoa zile zilizokufa, hivyo kupunguza ukavu na kutunza ngozi na kuifanya ingare na kuvutia. Mafuta ya shea ni kirutubisho muhimu kinachotumika kwa muda mrefu sana katika kutibu magonjwa mengi, hasa katika nchi za Afrika. Mafuta ya shea yana triglycerides ambayo ni muhimu katika kuleta unyevun na kulinda ngozi kwa muda mrefu. Karanga na vyakula jamii ya karanga vina vitamin E ambayo ni muhimu katika kuzuia kuzeeka kwa ngozi hasa kutokana na kupigwa sana na jua.
Vitamin E pia husaidia ngozi kuhifadhi unyevu na hivyo kuifanya ngozi kuwa inang'aa na nyororo. Vyakula vyenye kuimarisha afya ya ngozi ni vingi lakini hatutomaliza kuvitaja bila kuzungumzia nafaka zisizokobolewa ambayo sio tu ina faida kwa ngozi bali kwa mwili mzima. Mfano ngano isiyokobolewa ni chanzo muhimu cha Vitamin B ambayo inasaidia seli kutengeza mafuta na hivyo kuzuia ngozi kupasuka na kukatika kirahisi. Tunashauriwa pia kunywa maji kwa wingi ili kuifanya ngozi iwe nyororo.
Wapenzi wasikilizaji tunahitimisha kipindi chetu kwa kuelezea namna ya kutibu tatizo la ngozi linalowasumbua wengi la vipele usoni au chunusi. Kuna idadi kubwa ya watu wanaokabiliwa na tatizo la vipele vya usoni huku kuwa na chunusi kukiwa jambo lenye karaha sana, kwani huwafanya baadhi wapoteze mvuto wa asili na hata kuwakosesha raha. Lengo la tiba ya chunusi ni kupunguza uzalishaji wa mafuta ya sebum usoni pia kutibu vijidudu vya bakteria ambavyo hushambulia ngozi ya uso na kusababisha viupele vinavyowasha na wakati mwingine kuleta maumivu usoni.
Uchaguzi wa dawa hutegemea na jinsi ugonjwa ulivyoshambulia uso, sehemu iliyoharibika huhitaji kufanyiwa usafi wa kutosha kila siku tena uwe wa ziada zaidi ya kawaida kwa kutumia sabuni zenye antibaotiki, kubadilisha mazoea ya chakula, na pia matumizi ya kemikali za Sulfur salicylic acid na Resorcinol haisaidii kuondoa chunusi. Matibabu hugawanywa sehemu kuu tatu ambazo kwanza ni kwa wale wenye chunusi kidogo, pili wenye chunusi za wastani na tatu ni wale walioathirika sana yaani wenye chunusi nyingi.
Wale wenye vipele au chunusi kidogo hutumia dawa moja tu ambayo hujulikana kama Benzoyl peroxide au pia huchanganya na dawa ya antibaotiki, ambapo mgonjwa hutumia kila siku kwa kipindi cha wiki 6 na zaidi. Wale wenye chunusi za wastani huhitaji dawa za antibaotiki kama vile Tetracycline, Doxycline, Minocycline na Erythromycin. Dawa hizi hutumika kwa kipindi kisichopungua wiki 12 na hutolewa na daktari baada ya kuridhika kuwa haziwezi kumuathiri mgonjwa, kwa kuzingatia hali yake jumla ya kiafya. Hivyo tunaahauriwa kupata ushauri wa daktari kabl aya kutumia dawa hizo.
Kwa wale wenye chunusi nyingi dawa ya kunywa ya Isotretinoin ndiyo dawa sahihi inayopaswa kutumiwa na hutibu vizuri chunusi ambapo hutumika baada ya kupima uzito na kwa kipindi cha wiki 16 hadi 20. Dawa pia hii inapaswa kutumiwa baada ya ushauri wa daktari.