Kamishna Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili, Jaji Salome Kaganda
Kauli hiyo ya Jaji Kaganda inaendelea kuonyesha namna vigogo katika utumishi wa umma wanavyoendelea kuvunja kanuni na taratibu za Sheria ya Maadili ya Utumishi Umma namba 13 ya mwaka 1995.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya maadili kwa makatibu wakuu wa wizara na manaibu, jaji huyo mstaafu alisema Sheria ya Maadili inawataka viongozi wa umma kutangaza zawadi kubwa wanazopewa, lakini wamekuwa hawafanyi hivyo.
“Sijawahi kusikia mtu aliyewahi kutangaza zawadi kubwa tangu nilipoingia madarakani; iwe kutoka kwenye Bunge, Serikali au Mahakama,” alisema Jaji Kaganda.
Alisema sheria hiyo haizuii zawadi ndogondogo za kimila kama mbuzi, lakini ni jambo la ajabu kuona kiongozi anapokea kinyago kilichotengenezewa kwa dhahabu lakini bado anakiita ni zawadi ya kawaida.
“Hapana, hatuwezi kwenda hivyo lazima zawadi zote kubwa zitangazwe,” alisema jaji huyo aliyeteuliwa Desemba 4, 2010 na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuiongoza Sekretarieti hiyo akichukua nafasi ya Jaji Stephen Ihema.
Kutokana na maelezo hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki alisema kuanzia jana atahakikisha ofisi zote za Serikali zinakuwa na kitabu cha kusajili zawadi kubwa ili kuepusha kuendelea na uvunjwaji wa maadili.
Alisema amefurahishwa na namna Jaji Kaganda alivyoeleza kinagaubaga namna viongozi wa umma wasivyotangaza zawadi kubwa wanazopokea.
Hii ni mara ya pili kwa Jaji Kaganda kutumia fursa za ufunguzi wa semina za maadili kwa viongozi wa umma kuibua makosa yanayofanywa na vigogo hao baada ya mwezi uliopita kumweleza Majaliwa kuwa wapo mawaziri watano walioshindwa kuwasilisha fomu za tamko la mali na madeni na kiapo cha uadilifu, licha ya muda wao kupita.
Baada ya taarifa hiyo, Majaliwa aliwasilisha majina hayo kwa Rais John Magufuli naye akatoa agizo kwa mawaziri hao kujaza na kuwasilisha fomu hizo siku hiyohiyo.
Mawaziri hao ni January Makamba wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano) na naibu wake Luhaga Mpina, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga.
Jana, Jaji Kaganda alisema viongozi wengi wa umma wamekuwa wakikiuka maadili kwa kuwa na migongano ya masilahi na kazi zao kuhusishwa na rushwa, kutumia vibaya madaraka yao na kuwaonya kuwa katika Serikali ya sasa mambo si kama za zamani.
“Tumesikia malalamiko kuwa baadhi ya makatibu wakuu wana mahusiano na watumishi wa chini kama makatibu muhtasi ambao hawawakubali kwa mapenzi yao, bali kwa kuogopa kupoteza kazi. Lakini kumbukeni siku hizi hakuna ganzi utashtukia umetumbuliwa, usaha unamwagika,” alisema Jaji Kaganda.
Kuhusu uwajibikaji, Waziri Kairuki aliwataka watumishi wote wa umma kuongeza ufanisi badala ya kusubiri Rais, Waziri Mkuu au mawaziri wawatumbue majipu.
“Kila mtu asimamie kazi zake na kuchukua hatua, awe mkurugenzi, mkuu wa wilaya au mtumishi yeyote lazima kuwajibika,” alisema.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi alisema Serikali ya Awamu ya Tano ina dhamira ya dhati ya kujenga maadili ya utumishi wa umma, hivyo itaendelea kusimamia utendaji ili kupambana na rushwa na ulimbikizaji mali za umma.
“Iwapo Sekretarieti mnaona kuna mapungufu kwenye sheria za maadili mtueleze, Serikali ipo tayari kuzirekebisha ili kuondoa mwanya wa kuvunja maadili,” alisema Balozi Kijazi ambaye semina hiyo ilikuwa mkutano wake wa kwanza tangu aingie ofisini.
Alisema Serikali haina mchezo na wavunjaji wa maadili na kwamba asingependa wala hatafurahi “atokee mmoja wa makatibu wakuu au naibu katibu mkuu akawa jipu la kutumbuliwa”.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome alisema mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma ni jambo jema la kukumbushana uwajibikaji na kwamba iwapo sheria, sera na taratibu zitafuatwa ni vigumu kutokea matatizo.