F MBEYE CITY SASA YAMFURAHISHA PHIRI | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

MBEYE CITY SASA YAMFURAHISHA PHIRI

KOCHA Mkuu wa Mbeya City FC, Mmalawi Kinnah Phiri  amesema kwamba kwa sasa ana uhakika nyota wake wako kwenye kiwango kizuri kufuatia kufunga jumla ya mabao matano kwenye mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Phiri  amesema ushindi wa 4-0 dhidi ya Coastal Union na 1-0 dhidi ya Mgambo JKT mwishoni mwa wiki iiliyopita umempa matumaini makubwa juu ya wachezaji wake kwamba wameanza kuielewa vyema falsafa yake, hususan kwa kushinda bila  kuruhusu kufungwa bao hata moja katika michezo hiyo miwili.

"Tulianza kucheza kwa mchezo wa kawaida, sasa tumeongeza, tunacheza kwa kasi kubwa, wachezaji wangu sasa wanajiamini kwa kiwango kikubwa, tumefunga mabao matano bila kuruhusu kufungwa bao lolote, hili ni uhakika tosha kuwa kikosi changu sasa  kipo imara kwenye ulinzi na pia kipo vizuri kwenye ufungaji,"amesema.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Malawi, alisema kwamba mara baada ya kurejea  kutoka mjini Tanga kwenye mchezo dhidi ya Mgambo JKT, alitoa siku chache za mapumziko kwa wachezaji wake na kuwataka  kujiandaa kwa mazoezi yatakayoanza  siku ya Jumatatu tayari kwa mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uliopangwa kuchezwa mwishoni  mwa mwezi huu.

"Baada ya Tanga, nilitoa mapumziko ya siku saba, vijana watarejea Jumatatu tayari kwa mazoezi  kabla ya kuivaa Mtibwa, nina  imani siku saba  zitatosha  kuwaweka sawa kwa ajili ya mchezo huo, Sifahamu sana  kuhusu timu hiyo ya Morogoro, kwenye ratiba inaonyesha watacheza Jumamosi (na Yanga),".

"Nitatumia muda wangu kuangalia mchezo wao kwenye TV, nataka kujua baadhi ya mambo muhimu ili nijiandae  vizuri kuweza kupata ushindi,"amesema kocha huyo wa zamani wa Free State Stars ya Afrika Kusini.