F BARAZA LA TAIFA LA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI (NEEC) LASHAURIWA KUPANUA WIGO WA MAFUNZO YA UWEZESHAJI | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

BARAZA LA TAIFA LA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI (NEEC) LASHAURIWA KUPANUA WIGO WA MAFUNZO YA UWEZESHAJI

 Mkurugenzi wa Uwezeshaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bi. Anna Dominick akitoa mada wakati wa mafunzo ya siku tano kwa waratibu wa madawati ya uwezeshaji yaliyofanyika katika kanda ya kusini mkoani Lindi na kuhusisha mkoa wa Mtwara na kumalizika mwishoni mwa wiki.

Waratibu wa Madawati ya Uwezeshaji wakiwa kwenye majadiliano wakati wa mafunzo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyofanyika mkoani Lindi na kushirikisha mkoa wa Mtwara kwa kanda ya kusini.  Mafunzo hayo yaliratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi (NEEC).

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limeshauriwa kufanya semina elekezi kwa wananchi na viongozi wa kisiasa ili kuelimisha kuhusu dhana ya uwezeshaji.
Ushauri huo umetolewa na Mratibu wa Dawati la Uwezeshaji kutoka wilaya ya Liwale Bw. Moses Mkoveke wakati wa mafunzo ya uwezeshaji yaliyofanyika mkoani Lindi hivi karibuni.

“Elimu hii ikiwafikia viongozi wa kisiasa katika ngazi ya mkoa, halmashauri, mabaraza ya kata na hata vijiji itasaidia katika kuwajengea wananchi uelewa wa dhana ya uwezeshaji,” alisema Bw. Mkoveke.
Alisema hali hii italeta uelewa wa pamoja na hivyo kufanya sera ya uwezeshaji wananchi kutekelezeka kwa urahisi na ufanisi zaidi.
Aliongeza kusema kuwa elimu hiyo pia itasaidia kujenga uelewa kwa wananchi juu ya utaratibu wa upatikanaji na urejeshaji wa Tshs milioni 50 kwa kila kijiji kama ilivyoahidiwa na Rais John Magufuli.
Mratibu wa dawati hilo kutoka Wilaya ya Lindi, Bi.Yolenda Makumbuli alisema mafunzo hayo yamewapa mwanga wa namna ya kuunganisha wananchi katika vikundi vya ujasiriamali ili waweze kuibua fursa za biashara na kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

“Changamoto iliyopo ni kubadili mitazamo ya wananchi ili wawe wabunifu katika maeneo yao ili kujiletea maendeleo kiuchumi,” alisema Bi.Makumbuli.
Aliongezea kuwa ili kufikisha elimu ya uwezeshaji kwa wananchi, ushirikiano unahitajika toka kwa wadau wote wa maendeleo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uwezeshaji (NEEC) Bi. Anna Dominick alisema mafunzo yalikwenda vizuri na mwitikio kwa waratibu ulikuwa mkubwa na kuwa matarajio ya baraza hilo ni kwamba watakwenda kutekeleza waliyowafundishwa katika maeneo yao.

“Tunapata faraja kuona utayari waliokuwa nao waratibu wa kufanya kazi,” alisema Bi. Anna.

Alisema changamoto kubwa iliyopo katika mikoa ya kanda ya kusini ya Lindi na Mtwara ni mapato na wingi wa kata katika halmashauri, hali inayoweza kupelekea waratibu kutofanya kazi zao kwa ufanisi na ripoti kutofika kwa wakati.
Akizungumzia swala la ahadi ya Tshs Milioni 50 kwa kila kijiji alisema baraza litaendelea kutoa semina kuhusu fedha hizo na utaratibu utakaotumika katika kuwafikia wananchi.

Alisistiza kuwa fedha hizo sio zawadi bali ni mkopo ambao utatolewa katika kijiji kwa awamu ili ziweze kuwafikia wananchi wote katika kufanikisha shughuli za kiuchumi ili kupiga hatua kimaendeleo.
Mafunzo kwa waratibu wa madawati ya uwezeshaji yameshafanyika katika kanda ya nyanda za juu kusini katika mikoa sita ya Mbeya, Songwe, Ruvuma, Rukwa, Iringa na Njombe.
Wiki iliyopita yamemalizika katika kanda ya kusini mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo la kutoa mwongozo wa utekelezaji wa sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.