Dagaa inawatoa wengi Mwanza

Mwanza. Ni samaki wadogo lakini wenye umaarufu mkubwa siyo tu nchini, bali hata nje ya mipaka ya Tanzania.

Samaki hawa ni dagaa au Omena kama wanavyojulikana nchi jirani ya Kenya.

Kwa wakazi wa maeneo ya mwambao, neno dagaa siyo geni kwa sababu ni kati ya kitoweo kinachopatikana kirahisi na kwa bei nafuu.

Miaka ya nyuma, samaki hawa wanaovuliwa nyakati za usiku kwa kutumia mwanga wa taa za karabai walikuwa wakitumika nchini pekee.

Lakini hivi sasa, ni bidhaa maarufu nje ya mipaka nchi kama anavyosema, Fikiri Magafu, Mwenyekiti wa Soko la Kimataifa la Samaki la Kirumba jijini Mwanza.

“Soko la dagaa kutoka Mwanza limetanuka hadi nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Zambia na Kenya,” anasema Magafu.

Dhahabu ndani ya Ziwa Victoria
Magafu anasema wakati Serikali mkoani Mwanza inaweka mikakati ya kukuza sekta ya madini ya dhahabu yanayopatikana sehemu mbalimbali mkoani humu, ni vyema ikakumbuka pia kwamba uvuvi wa dagaa nao ni dhahabu inayopatikana ndani ya Ziwa Victoria.

“Ikitiliwa maanani kuanzia kwa wafanyabiashara wenyewe na mamlaka nyingine, biashara ya dagaa inaweza kuwa miongoni mwa fursa na vyanzo vikuu vya mapato na uchumi wa Mkoa wa Mwanza,” anasema.

Miaka ya nyuma samaki hawa wadogo waliuzwa baada ya kukaushwa kwa juu. Lakini hivi sasa teknolojia ya kuwaandaa imekuwa kiasi kwamba wapo dagaa ‘tayari’.

Hawa ni dagaa waliopembuliwa, kuchambuliwa na kukaushwa vyema kwa mafuta tayari kwa kuliwa.

“Watu wengi huwatumia dagaa wa aina hii kama kiburudisho kwa kuwatafuna hata maofisini,” anasema Magafu.

Hata hivyo, ubora wa samaki hawa bado ni changamoto kuanzia kwenye kuvuliwa hadi kuanikwa kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuendelea na mtindo wa kuwaanika chini kwenye mchanga na hivyo kupunguza ubora wake kwani huchanganyika na mawe au mchanga.

Bado kuna fursa ya kuwekeza katika sekta hii kwa kuwajengea uwezo wavuvi ili kuvua kwa tija na pia wafanyabiashara kwa kuwapa elimu na mitaji itakayowawezesha kukidhi mahitaji ya soko la ndani la kimataifa.

Jitihada za FAO kwa dagaa
Magafu anasema umuhimu wa dagaa kwa lishe na uchumi wa taifa unathibitishwa na uamuzi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), kutoa waraka maalumu kuhusu Uvuvi Endelevu (Code of Conduct for Responsible Fisheries), kwa lengo la kupunguza upotevu wa samaki na dagaa kwa kuhakikisha kitoweo hicho kinakuwa salama kwa soko zuri.

FAO imebuni mradi wa gharama nafuu wa ukaushaji nafuu wa samaki na dagaa kwa kuanika kwenye vichanja, mradi unaotekelezwa pia katika mwambao wa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.

Dagaa zinalipa
Mfanyabiashara wa dagaa eneo la Buhongwa, Mwanza, Ester Simon anasema gunia moja la dagaa linauzwa kati ya Sh120,000 hadi Sh130, 000 kulingana na ubora.