Dar/Shinyanga. Matokeo ya darasa la saba mwaka huu yameacha kicheko kwa Shule ya Msingi Kwema Modern iliyopo Kahama mkoani Shinyanga, baada ya kuibuka mshindi wa kwanza kitaifa.
Shule hiyo imefanya maajabu kwa kutoa wanafunzi saba katika orodha ya watahiniwa 10 bora kitaifa.
Hata hivyo, wanafunzi 238 wamefutiwa matokeo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya baadhi ya wasimamizi wa mitihani, wamiliki wa shule na walimu wakuu kuwapatia majibu na kubainika kuwa yanayofafana.
Pia, wanafunzi 21 watarudia mitihani yao kutokana na sababu mbalimbali kama maradhi.
Akitangaza matokeo hayo jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alisema watahiniwa 555,291 (sawa na asilimia 70.36) wamefaulu kati ya 789, 479 waliofanya mtihani huo Septemba mwaka huu.
Matokeo hayo yanaonyesha kiwango cha ufaulu mwaka huu kimepanda kwa asilimia 2.52 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2015 ambao ulikuwa asilimia 67.84.
Mbali ya Kwema kuwa shule ya kwanza kwa matokeo ya jumla, imetoa mtahiniwa bora wa kwanza kitaifa.
Mtahiniwa huyo, Japhet Elia (12) ambaye anatoka familia ya wakulima mkoani Kigoma, amefuatiwa na wenzake wawili, Jamal Ally na Enock Daud pia wa shule hiyo walioshika nafasi ya pili na tatu.
Dar, Shinyanga zachuana
Tofauti na matokeo ya mwaka 2015 ambayo shule za Kanda ya Ziwa zilitamba, mwaka huu mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga imechuana vikali.
Kwa mujibu wa Dk Msonde, Dar es Salaam imeibuka kinara kwa kutoa shule nyingi katika orodha ya shule 10 bora, huku Shinyanga ikiongoza kwa kutoa wanafunzi wengi bora kitaifa.
Alisema Dar es Salaam imetoa shule nne kati ya 10 bora, ikifuatiwa na Shinyanga yenye shule mbili.
Katika orodha ya wanafunzi bora kitaifa ambayo mwaka huu imetawaliwa na wahitimu tisa wa kiume na mmoja wa kike, Shinyanga imeongoza kwa kutoa wanafunzi saba kati ya 10. Dar es Salaam imefuatia kwa kutoa wahitimu wawili na Kagera mhitimu mmoja.
Mikoa hiyo pia imechuana vikali katika orodha ya wanafunzi bora kitaifa kwa jinsia. Wakati Dar es Salaam ikitoa wanafunzi watano kati ya kumi kwa upande wa wasichana, Shinyanga imeongoza kwa wavulana kwa kutoa wanafunzi wanane.
Shule 10 bora
Dk Msonde alizitaja shule 10 bora kwa kigezo cha kuwa na wanafunzi 40 na zaidi kuwa ni Kwema (Shinyanga), Rocken Hill (Shinyanga), Mugini (Mwanza), Fountain of Joy (Dar es Salaam), Tusiime (Dar es Salaam), Mudio Islamic (Kilimanjaro), Atlas (Dar es Salaam), St Achileus (Kagera), Gift Skillfull (Dar es Salaam) na Carmel (Morogoro).
Shule zilizofanya vibaya ni Mgata (Morogoro), Kitengu (Morogoro), Lumba Chini (Morogoro), Zege (Tanga), Kilole (Tanga), Magunga (Morogoro), Nchinila (Manyara), Mwabalebi (Simiyu), Ilorienito (Arusha) na Chohero (Morogoro).
Ushirikiano siri ya ushindi
Mkurugenzi wa Shule ya Kwema Modern, Pauline Mathayo alisema mafanikio waliyopata yanatokana na ushirikiano wa karibu uliopo shuleni hapo kati ya walimu, wazazi na wanafunzi.
Pia, alitaja siri nyingine kuwa ni kufuata miongozo ya elimu wanayopewa na Serikali.
Baba, mwana washangaa
Katika kile kinachoonekana ni kutoamini kilichotokea, Elia Stephano, mzazi wa mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa, alisema hakutegemea kama mwanawe angeweza kupata mafanikio hayo makubwa, licha ya kuwa amekuwa na nidhamu kubwa tangu akiwa mdogo.
“Ukweli baada ya kuelezwa hivyo kwamba mtoto wangu amekuwa wa kwanza kitaifa, nilianza kutetemeka kwa furaha,” alisema Stephano anayejishughulisha na kilimo na ujasiriamali mkoani Kigoma.
“Hayakuwa mategemeo yangu ingawa nilikuwa namwamini mtoto wangu. Lakini si kwa kiasi cha kuwa mshindi wa kwanza kitaifa.”
Alisema mtoto wake anapenda kusoma na kufundisha wenzake huku mara nyingi akipenda kumuomba Mwenyezi Mungu.
Mtoto aliyeongoza kitaifa, Japhet alisema pamoja na kufanya vizuri kwenye mitihani alipokuwa akisoma, hakuwa na matarajio ya kushika nafasi ya kwanza.
“Namshukuru Mungu kwa matokeo hayo. Pia, nawaomba watoto wenzangu katika mambo yao yote wamtangulize Mungu kwa kila jambo hata kama wana uwezo binafsi,” alisema Japhet huku akieleza kuwa ndoto yake ni kuwa mhandisi wa ndege.
Tusiime wazungumza
Akizungumzia matokeo ya mwanafunzi wa kike aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa kwa wasichana Justina Gerald, mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Tusiime, Philibert Simon alisema siri ya mwanafunzi huyo kufanya vizuri ni usikivu, nidhamu na uchu wa kujifunza.
Simon alisema msichana huyo ambaye pia ameshika nafasi ya nne kitaifa, alikuwa akifanya vizuri katika mitihani yake shuleni hapo.
Alisema wakati akiwa darasa la saba aliongoza mara 19 katika mitihani 32 waliyofanya wanafunzi hao. Akishuka sana amekuwa wa pili,” alisema Simon.
Udanganyifu
Licha ya ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.5 katika mitihani ya darasa la saba, matokeo yametiwa dosari na udanganyifu uliojitokeza wakati wa uendeshaji wake.
Msonde alisema wakati wa mitihani hiyo, matukio machache ya udanganyifu yalifanywa na baadhi ya wasimamizi, wamiliki wa shule na walimu wakuu.
Udanganyifu uliofanyika unahusisha wamiliki na walimu wa shule kuiba mtihani na kuandaa majibu kwa ajili ya wanafunzi, walimu kuwasaidia wanafunzi kufanya mtihani, walimu kuwapa majibu wanafunzi na kufanana kwa majibu kusiko kwa kawaida.
Kwa mfano, katika shule ya Tumaini, Sengerema mkoani Mwanza, mmiliki wa shule aliandaa majibu ambayo watahiniwa waliandika kwenye sare za shule na kuyatumia ndani ya chumba cha mitihani.
Katika shule ya Mihamakumi wilayani Sikonge, mwalimu mkuu na walimu wengine waliwafanyia watahiniwa mitihani lakini baadaye maafisa wa Takukuru waliwakamata.
Msonde alisema tukio jingine la udanganyifu lilifanywa Shule ya Msingi Qash wilayani Babati, Manyara ambapo mwalimu alijificha chooni, kupokea maswali kutoka kwa watahiniwa na kuandaa majibu ili kuwapa wanafunzi.
Katika shule ya St Getrude mkoani Ruvuma, mwalimu mkuu na walimu wengine walijificha mabwenini na watahiniwa walijifanya wanaomba ruhusa ya kwenda chooni, kisha walienda mabwenini kuchukua majibu na kuyasambaza ndani ya chumba cha mtihani.
Shule nyingine zilizohusika katika udanganyifu huo ni Tumaini iliyopo Halmashauri ya Sengerema (kuiba mtihani na kuandaa majibu), Little Flower Halmashauri ya Serengeti (kuiba mitihani na kuandaa majibu).
“Necta imewafuta matokeo yote watahiniwa 238 kutoka shule sita za mikoa tofauti tofauti waliobainika kufanya udanganyifu na tumezishauri mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua wote waliohusika kulingana na kanuni za utumishi na sheria za nchi,” alisema Msonde.
Aliongeza kuwa Necta haitamvumilia mtumishi yeyote anayevunja kanuni na sheria za nchi kwa kuvuruga usimamizi wa mitihani ya Taifa.
Imeandikwa na Shija Felician, Suzan Mwillo na Ephrahimu Bahemu.
Source: Mwananchi