Mamlaka ya Chakula na Dawa ( TFDA ) Kanda ya Ziwa imekamata kilo 200 za dawa za binadamu ambazo hazina usajili pamoja na kilo tano za dawa bandia zenye thamani ya jumla ya shilingi milioni sita,katika ukaguzi hakiki uliofanyika kwenye Halmashauri tano za mkoa wa Mwanza.
Dawa hizo zimekamatwa kati ya Oktoba 18 na Novemba Mosi mwaka huu katika Halmashauri za wilaya ya Ukerewe,Kwimba,Misungwi,Sengerema na Buchosa zikiwa zinauzwa kwenye baadhi ya maduka ya dawa muhimu,hospitali na zahanati,ambapo mkaguzi wa dawa Kanda ya Ziwa wa TFDA Mtani Njegere amesema watu 6 waliokamatwa na dawa bandia maduka yao yamefungwa,huku maduka 16 yaliyokutwa yakiuza dawa zisizo na usajili yamelipa gharama za uteketezaji.
Mfamasia wa mkoa wa Mwanza Tuloson Nyalaja, pamoja na Afisa Afya wa mkoa huo Fungo Masalu,wamewataka wakaguzi wa halmashauri za wilaya mkoani hapa kufanya kaguzi za mara kwa mara katika maeneo yao na kuwa na mpango kazi wa mwaka kwa ajili ya kuondoa bidhaa zisizokidhi matakwa ya sheria ya chakula na dawa namba 1 ya mwaka 2003 ili kulinda afya za walaji.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya misungwi eliud mwaiteleke amemuagiza afisa afya wa halmashauri hiyo kuanzia novemba 3 mwaka huu,kuhakikisha anamkabidhi ratiba ya mpango kazi inayoonesha namna idara hiyo ya afya wilayani humo ilivyojipanga katika kutekeleza zoezi hilo lililoanzishwa na tfda.