Akizungumza wakati wa mazishi ya mtoto wake, mzazi wa kijana huyo, Juma Sleym, alisema kabla ya kuuawa Isihaka alikodiwa na watu wasiojulikana Desemba 10, mwaka huu, lakini hakurudi tena mpaka Desemba 11, mwaka huu bajaji yake ilipoonekana ikiwa pembezoni mwa barabara kuu ya lami.
Alisema baada ya kuiona bajaji hiyo walianza kumtafuta mtoto wake na kuupata mwili wake ukiwa umefichwa kichakani huku shingo ikiwa imenyongwa na kichwa kikiwa kimepigwa kwa kitu kizito.
Kufuatia tukio hilo, wananchi waligoma kuuzika mwili wa marehemu, wakimtaka Mkuu wa Polisi Igunga, Mayala Kepha, kwenda msibani hapo ili atoe maelezo juu ya matukio ya kuuawa waendesha bajaji kushamiri na kushindwa kuwakamata wauaji.
Hata hivyo, baada ya umati huo kumsubiri mkuu huyo wa polisi kwa muda mrefu bila mafanikio, walikwenda barabara kuu ya lami ilipokutwa pikipiki ya marehemu na kufunga barabara kwa kuweka mawe, magogo na matawi ya miti.
Hali hiyo ilisababisha magari zaidi ya 400 kutoka Dar es Salaam na Mwanza kukwama katika eneo hilo kuanzia saa 6:15 hadi saa 11:00 jioni hadi pale polisi wilaya ya Igunga walipoenda kuwatawanya kwa kupiga mabomu ya machozi mfululizo, lakini bila ya mafanikio na kulazimika kuomba msaada wa kuongezewa askari wengine kutoka mkoani Tabora.
Baada ya polisi kupiga mabomu kwa wingi, wananchi hao walitawanyika na kuwezesha magari yaliyozuiliwa kuendelea na safari zao.
Baadhi ya madereva waliokwama katika eneo hilo, Selemani Issa na Salum Hussein, walisema ni vyema Jeshi la Polisi likakaa meza moja na wananchi wa Igunga ili kudhibiti matukio kama hayo yasijirudie.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi walioshiriki mazishi ya mwendesha huyo bodaboda, Ramadhani Hussein, Moshi Haruna, Ras Karetus walisema wameamua kufunga barabara kwa sababu Agosti, mwaka huu aliuawa mwendesha bajaji mwingine, Alex Okungu, lakini polisi Igunga wameshindwa kuwakamata wahalifu na kumtaka waziri wa mambo ya ndani ya nchi amuondoe mkuu wa polisi wilayani humo.
Diwani wa Kata ya Igunga, Charles Bomani, alisema wananchi walikuwa watulivu, lakini kutofika kwa mkuu polisi ndiyo kuliwaongezea machungu na kuamua kwenda kufunga barabara na kuongeza kuwa yeye kama diwani hayuko tayari kuona wananchi wake wakipoteza maisha huku polisi wakishindwa kuwakamata wauaji.
Naye Mbunge wa Manonga, Hamis Seif Gulamali, alisema polisi hawakupaswa kutumia nguvu kubwa kwani wananchi hao wasingechukua hatua hiyo endapo mkuu huyo wa polisi angefika kwenye msiba na kuzungumza nao na kwamba suala hilo ameliwasilisha katika mamlaka husika ili kujua ufumbuzi wake.
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Marchades Magongo, amethibitisha kupokea mwili wa kijana huyo na kusema kuwa chanzo cha kifo chake ni kutokana na ubongo kutikisika kutokana na mashambulizi aliyoyapata.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamisi Issa, ili kuzungumzia tukio hilo hazikuzaa matunda baada ya kupigiwa simu yake ya mkononi bila ya kupokelewa.