Bukoba. Watu wawili wameuawa na wananchi waliojichukulia sheria mkononi kwenye Kijiji cha Nyabihanga wakiwatuhumu kwa wizi wa mbuzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Agustino Olomi alisema kuwa miili ya watu hao, Audax Mushumbusi (25), aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Kanazi na Sadoki Ernest (15), mkazi wa Kijiji cha Djululigwa, ilitelekezwa kwenye korongo.
“Tunawashikilia wananchi saba, wakiwamo viongozi wa Kijiji cha Nyabihanga kwa upelelezi ili kubaini waliohusika na mauaji ambao watafikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema Olomi.
Katika tukio jingine, alisema mwanamke mkazi wa Kijiji cha Mumuhamba wilayani Ngara, Efrazia Thadeo (50), alikutwa akiwa amekatwa pua na mdomo, mwili wake ulipokuwa ukipelekwa chumba cha kuhifadhia maiti baada ya kufariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rulenge.
Alisema Thadeo alifikishwa hospitalini hapo Desemba 18, akisumbuliwa na maradhi ya homa na kisukari. Alisema ndugu zake waliompeleka hospitali walitoweka.