F Makubwa yaibuka mauaji ya kinyama | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Makubwa yaibuka mauaji ya kinyama

KATIBU MKUU WA CHAMA CHA WAFUGAJI, MAGEMBE MAKOYE

MAMBO makubwa yameibuka katika mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na askari wa Suma JKT mkoani hapa katikati ya wiki na kuua watu watano.

Katika tukio hilo imebainika kuwa mtoto wa miaka 13 ambaye ni miongoni mwa majeruhi katika tukio hilo (jina tunalihifadhi), amepoteza mawasiliano katika viungo vyake vya mwili.

Aidha, asasi na wanaharakati wamejitokeza kukemea kitendo hicho cha askari hao.

Taarifa za kitabibu kutoka katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, zimeeleza kuwa hali hiyo inatokana na risasi kuingia katika uti wa mgongo.

Mtoto huyo sasa amehamishiwa Hospitali ya Rufani ya KCMC, Moshi kwa matibabu zaidi.

Mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu, ni mmoja wa watu saba waliojeruhiwa katika mashambulizi hayo yaliyosababisha vifo vya watu watano kwa kupigwa risasi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alifika hospitalini hapo jana na kuelezwa habari za kuhamishwa kwa mwanafunzi huyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, juzi aliwataja watu waliofariki dunia kutokana na tukio hilo kuwa ni Mbayani Melau (27) ambaye ni mfugaji na mkazi wa kijiji cha Kandaskirieti, Julius Kilusu (45) mkulima na mkazi wa Kandaskirieti, Lalashe Meibuko (25) mkulima na mkazi wa Kandaskirieti na Seuri Melita (32) mkazi wa Olkokola.

Taarifa za kifo cha tano zilitolewa na Diwani wa Kata ya Odonyosambu, Raymond Lairumbe, ambaye alisema alifariki akipatiwa matibabu hospitalini ingawa hakuweza kutaja jina lake mara moja.

Mbali na mwanafunzi huyo, wengine waliojeruhiwa kwa kushambuliwa kwa risasi na askari hao waliokuwa wakilinda Msitu wa Hifadhi ulioko eneo la Mlima Meru, wilayani Arumeru ni William Ngirangwa (29) na Mathayo Masharubu (34).

Wengine ni Julius Lazaro (32) na Evalyn Melio (28) wote wakazi wa Kijiji cha Kandaskirieti.

Akizungumza mbele ya Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Maghembe, Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Elias Mashala, alisema walipokea majeruhi wanne wa risasi Januari 24, mwaka huu.

"Lakini majeruhi watatu risasi hazijaingia katika mifupa, hivyo tumeamua kuziacha mwilini mwao, kwani hazitakuwa na madhara isipokuwa majeruhi mwanafunzi huyu tumelazimika kumhamishia KCMC sababu risasi ilimpiga katika uti wa mgongo na muda unavyokwenda anakata mawasiliano na sehemu zingine za mwili,” alisema Dk. Mashala.

Alisema mtoto huyo hana hisia anapofinywa miguu na kwa sababu Mount Meru haina vipimo vikubwa, wamelazimika kumhamishia KCMC.

Dk. Mashala alisema wagonjwa wengine watawaruhusu kwenda nyumbani kwa kadri hali zao zitakavyoendelea kuimarika.

SERIKALI ITAGHARAMIA
Kwa upande wake, Waziri Maghembe alisema lengo lake ni kuona hali za wagonjwa na kuagiza kupata mawasiliano yao, ili watakaporuhusiwa kwenda nyumbani awafuatilie kwa karibu kuona hawapati madhara yoyote.

Alisema tukio hilo linasikitisha na polisi wanalifanyia uchunguzi, kisha hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
"Serikali itagharimia matibabu na tunawapa pole waliopatwa na mkasa huu," alisema Prof. Maghembe.

"Tunaomba uvumilivu, tuache vyombo husika kwa uchunguzi."

Juzi, Jeshi la Polisi mkoani hapa, lilithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai askari wa Suma JKT wanashikiliwa kwa uchunguzi wa tukio hilo.

Kamanda Mkumbo alisema chanzo cha mauaji hayo ni wafugaji wa jamii ya Kimasai kuwavamia askari hao ambao walikuwa wamekamata ng’ombe wao waliokuwa wameingizwa ndani ya msitu wa hifadhi, ambao ni mali ya serikali.

Inadaiwa kuwa walifanya hivyo kutokana na ukosefu wa malisho kwa sababu ya ukame mkubwa unaoendelea katika maeneo mengi mkoani hapa.

Alisema askari hao ambao wanalinda msitu huo, maarufu kama 'Shamba la Miti la Meru Usa Plant', walianza operesheni yao Jumanne ili kuondoa mifugo iliyoingizwa ndani ya msitu huo.

Kamanda Mkumbo alisema wakiwa katika operesheni majira ya asubuhi, askari wa Suma JKT walikamata ng’ombe 45, mbuzi na kondoo 65 na kuwapeleka kwenye zizi maalumu lililoko kituo cha polisi Oldonyosambu.

Alisema askari hao waliendelea na operesheni hiyo na ilipofika saa 8:00 mchana walipata taarifa kuwapo kwa kundi lingine la mifugo katika msitu huo na kukamata ng’ombe 80, mbuzi na kondoo 70 kwa lengo la kuwapeleka kwenye zizi hilo.

"Wakati wanaswaga mifugo hiyo," alisema wananchi wakiwa na silaha za jadi walijitokeza mbele yao wakitaka kukomboa mifugo kwa nguvu.

Hatua hiyo ilisababisha askari nao kuanza kuwafyatulia risasi na kusababisha vifo vya vijana wanne na watano kujeruhiwa.

Wakati huo huo, Diwani wa Kata ya Odonyosambu, Raymond Lairumbe, jana alisema viongozi wa serikali wamefika kijijini hapo na kuzungumza na wananchi ambao amekubali kuzika miwili ya wapendwa wao leo.

Alisema miili mitatu itazikwa Kata ya Olkokola na mmoja Oldonyosambu.

"Kikubwa tumefika uamuzi wa kuzika baada ya kuona serikali imewashikilia askari sita hadi sasa na hili linatupa imani wako pamoja na sisi," alisema.

Serikali ya Wilaya ya Arumeru iliwaomba wananchi waliopoteza wapendwa wao katika tukio hilo, kukubali kuichukua miili ya marehemu kwa maziko yatakayogharimiwa na serikali.

Serikali ilisema imesikitishwa na tukio hilo na itaungana na wananchi hao katika maziko hayo yanayotarajiwa kufanyika leo.

Diwani Lairumbe alisema wananchi wamekubali kushirikiana na serikali katika shughuli hiyo ya maziko na amewaomba wafiwa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Jijini Dar es Salaam, Chama cha Wafugaji na asasi zinazojishughulisha na masuala ya wafugaji zimetoa tamko la kulaani tukio la askari wa Shirika la Uchumi la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) kuwaua kinyama kwa kuwapiga risasi wafugaji wakazi wa Oldonyosambu, wilaya ya Arumeru mkoani Arusha baada ya kuingiza mifugo ndani ya Msitu wa Hifadhi ya Mlima Meru.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Magembe Makoye, akizungumza jana jijini Dar es Salaam ameitaka Wizara ya Kilimo na Mifugo kutoa tamko juu ya migogoro ya ardhi inayoendelea nchini kati ya wafugaji na watumiaji ardhi wengine pamoja na matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu wanayofanyiwa wafugaji inahatarisha amani ya nchi.

Makoye alisema kuwa wamesikitishwa na mwendelezo wa matukio ya ukandamizaji wanayofanyiwa wafugaji yanayosababisha vifo vyao na mifugo pamoja na majeruhi.

“Kabla ya uhuru ufugaji unatambulika kama shughuli nyingine yoyote kwa kuwa mfugaji ana tegemea kujipatia kipato na kuwa na idadi kubwa ya mifugo si dhambi kwani kuna watu ambao wanamiliki magari na nyumba nyingi hawajaambiwa wauze mali zao,”alisema.

Wizara ya Mifugo, alisema, inatakiwa kuweka mikakati ya kutenga maeneo rasmi kwa ajili ya malisho na suala la migogoro ya mifugo itamalizika nchini kwa kuwa wakulima watakuwa na eneo lao pamoja na hifadhi haitaingiliwa.

Mkurugenzi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Francis Nzuki, alisema kuwa tukio lolote linalosababisha kupoteza uhai wa binadamu ni kinyume cha haki za binadamu, na kwamba tume ina laani kitendo hicho.

“Amani tuliyokuwa nayo nchini kwa miaka yote tunajiuliza itakuwaje kwa miaka ya baadaye iwapo matukio kama haya yanataendelea kujitokeza kila siku?" Alisema.

"Tume mwaka jana ilifanya utafiti katika mikoa mbalimbali na kubaini kuwa migogoro ya ardhi inasababishwa na dosari za kuainisha matumizi rasmi ya ardhi.”

Imeandikwa na Cynthia Mwilolezi na Allan Isack, ARUSHA na Frank Monyo na Christina Mwakangale, DAR