Katika hali isiyo ya kawaida mamia ya wananchi wa kijiji cha Mwakizega tarafa ya Ilagala wilayani Uvinza mkoani Kigoma wameandamana na kufunga siku nzima Zahanati ya kijiji kupinga uhamisho wa muuguzi pekee katika zahanati ya kijiji kutokana na jinsi anavyowahudumia wagonjwa vizuri.
Wameeleza kuwa wamechukua maamuzi hayo ili kueleza hisia zao kutokana na muuguzi huyo Zainab Hassan kupewa uhamisho kwenda zahanati ya kijiji cha Sunuka, hali ambayo itaathiri upatikanaji wa huduma za afya huku kaimu afisa mtendaji kata ya Mwakizega Mariam Ulimwengu akieleza kuwa huduma zilisimama baada ya kufungwa kwa kituo na wananchi licha ya kwamba kuna watumishi wengie wawili.
Kutokana na hali hiyo mbunge wa jimbo la Kigoma kusini Husna Mwilima na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Uvinza Jackson Mateso wamelazima kutumia hekima kubatilisha maamuzi hayo na kuonya watumishi wanaonyanyasa wagonjwa.