Mmoja wa viongozi wakuu wa kiislamu nchini Nigeria anasema kuwa atatangaza sheria ambayo itawazuia wanaume kuoa zaidi ya mke mmoja.
Kiongozi huyo kutoka jimbo la Kano Lamido Sanusi, anasema kuwa tamaduni ya kuoa wake wengi imechangia kuwepo ugaidi kaskazini mwa nchi.
Dini ya kiislamu inamruhujsu mwanamume kuoa hadi wake wanne.
Lakini kiongozi huyo anasema kuwa baadhi ya wanaume wa kiislamu hawana uwezo wa kutunza familia kubwa.
"Wanazaa watoto ishirini, watoto hawapati elimu na huishia kuwa wahalifu na magaidi." Alisema Sanusi.
Umaskini unaonekana kuwa sababu kuu ya kuibuka kwa kundi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Sanusi anasema kuwa sheria hiyo itakuwa sehemu ya sheria ya kifamilia ambayo itaharamisha ndoa za lazima.