F Walioongoza kidato cha nne wavutiwa na Obama, Trump | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Walioongoza kidato cha nne wavutiwa na Obama, Trump

WANAFUNZI walioongoza kitaifa katika matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa wiki hii, Alfred Shauri na Cynthia Mchechu wameshauri serikali kubadili mitaala na kuandaa wanafunzi katika kujiajiri huku kukiwa na aina moja ya vitabu kwa madarasa yote katika kufundisha wanafunzi wote nchini.

Aidha, wanafunzi hao kila mmoja ameonesha kuvutiwa na marais wa Marekani wakati Mchechu akieleza kuwa alivutiwa na aliyekuwa Rais wa 44 wa taifa hilo kubwa duniani, Barrack Obama na kuwa na ndoto ya kuwa mwanasheria, Shauri anavutiwa na Rais wa sasa, Donald Trump kwa jinsi anavyosimamia kile anachokiamini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walipofanya ziara ya kutembelea ofisi za Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha Daily News, SundayNews, HabariLeo, HabariLeo Jumapili na SpotiLeo,wanafunzi hao wametaka Serikali kuwaangalia wanafunzi waliofeli katika mitihani hiyo wasiishie mitaani.

Cynthia ambaye ni mshindi wa pili kitaifa na wa kwanza kitaifa kwa wasichana akitokea Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St. Francis mkoani Mbeya, alisema siyo sahihi kwa sasa kuwa na vitabu tofauti kwani mwingine anaweza kupata na mwingine kukosa, ni vema kuwa na vitabu vya aina moja.

Alisema ni vema serikali kuwasaidia wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na kufanya vibaya kwa kuangalia vipaji walivyo navyo kwa lengo la kuwapeleka katika vyuo vya ufundi na kwingineko.

Pia alisema ni vema kuongeza shule katika maeneo yasiyokuwa nazo huku walimu wakiwezeshwa ili kujituma katika kufanya kazi zao, kwani kuna walimu wameishi maeneo ya mjini na kupelekwa katika sehemu hakuna maji safi na umeme.

“Mimi naona Serikali ijitahidi kuwa na ‘standard’ ya vitabu kwani kwa sasa kuna vitabu vingi ambavyo ni vigumu wanafunzi kupata vyote hivyo anasoma kingine na maswali yanatoka vingine,” alieleza mshindi huyo wa kwanza kwa wasichana.

Msichana huyo wa pekee katika familia ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu, alisema Obama amechangia kuwa na ndoto kuwa mwanasheria baada ya kufuatilia historia yake.

“Kumwamini Mungu pia ni siri kubwa ya mafanikio yangu, uhusiano mzuri kwa watu wote wanaonizunguka pamoja na juhudi za walimu waliotujengea mazingira ya kuhakikisha tunafaulu,” alisisitiza.

Aliwashauri wasichana kusali na kufunga nyakati zote kwa ajili ya kuomba afya njema na kufanya vizuri nyakati za mtihani, kwani tatizo la vijana wengi wanasahau kuwa kuna muda wa kufanya yale unayotaka kufanya sasa, wakati muda wake bado, ni vema kuacha na kusubiri.

Shauri ambaye ni mshindi wa kwanza kitaifa akiwa mwanafunzi wa Sekondari ya Feza Boys ya jijini Dar es Salaam, anaitaka serikali kuangalia mitaala ili kusaidia hata wanafunzi watakaomaliza kidato cha nne au sita kutumia elimu yao katika jamii.

Alisema mitaala hiyo itasaidia waliofeli kutozagaa mitaani, bali kuwa na fani bila kusubiri kufika chuo kikuu.

Alisema siri kubwa ya mafanikio yake ni kujiamini, na kwamba kidato cha tano atasomea mchepuo wa PCM (Fizikia, Kemia na Hisabati) ili baadaye awe mhandisi wa umeme katika viwanda kwa lengo la kutengeneza mashine za viwanda kwani anatarajia kuwa mwekezaji katika sekta hiyo barani Afrika.

Aliwashauri vijana kuangalia namna ya kutumia mitandao ya kijamii kwani si mibaya katika kuendana na mabadiliko duniani, lakini tatizo ni muda mwingi wanaotumia kuwekeza katika mitandao hiyo hasa kwa wanafunzi.