Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemshauri msanii wa singeli Manfongo, kutumia lugha za misamiati na mafumbo katika kazi zake ili kuepusha maneno ya mtaani ambayo yanatafsirika kwa kuwa muziki huo unasikilizwa na watu wa rika tofauti.
Manfongo leo akiwa kwenye kipindi cha ‘Planet Bongo’ cha East Africa Radio amesema baada ya muziki wa singeli kuonekana kushika kasi sana BASATA walimtaka kutumia misamiati ambayo haijakaa kihuni huku wakitolea mfano mistari iliyomo kwenye wimbo wa 'Hainaga Ushemeji'.
“Katika wasanii wote wa singeli peke yangu ndiyo nmejiandikisha BASATA, baada ya kutoka India kwenye 'Show' wakaniita kwa sababu mimi ndiyo msanii wa singeli mwenye tuzo, wakanambia sasa Manifongo wewe umeshakuwa msanii mkubwa tafadhali kwenye hizi nyimbo zenu inabidi ukawe balozi wa kuwashauri wenzako mtumie maneno ya kiswahili yenye mafumbo, kiswahili mnachotumia kipo wazi sana kama hainaga ushemeji ndo nini?”. Alieleza Manifongo.
Aidha Manfongo amewaambia watangazaji wa kipindi hicho Dullah pamoja na Jay R Junior kwa sasa anataka kufanya yale aliyoagizwa kutoka BASATA kwenye kazi zake nyingine ili aweze kuwashawishi vijana wanaomtazama kama mfalme wa Singeli waweze kuelewa maneno gani ya kutumia kwenye muziki huo.
Pia msanii huyo ameweka wazi kuachana na uongozi wake wa mwanzo ambao umeshindwa kuwekeza kwake ikiwa ni pamoja na kushindwa kusimamia kazi yake ya Kibaka aliyoitoa siku zilizopita na kushindwa kufanya vizuri.