Shehena ya mbao zilizovunwa kinyume cha sheria zakamatwa Kilwa Kivinje

Na. Ahmad Mmow.
Msako mkali unaoendelea kufanyika wilayani Kilwa mkoani Lindi,umefanikisha kukamatwa mbao zilizovunwa kinyume cha sheria Kilwa Kivinje.

Akizungumza akiwa katika eneo ambalo mbao hizo zimehifadhiwa, mkuu wa wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai, amesema msako mkali unaoendelea wilayani humo wenye lengo la kuzinusuru maliasili zinazovunwa na kusafirishwa kinyume cha sheria, umefanikisha kukamatwa mbao takribani 2700 katika mji wa Kilwa Kivinje.

Zikiwa zimehifadhiwa katika maeneo tofauti ikiwa ni maandalizi ya kuzisafirisha kwa kutumia bandari bubu zilizopo katika mji mkongwe huo. Alisema licha ya kukamatwa kiasi hicho  cha mbao lakini pia vyombo hivyo vya ulinzi vinalishikilia lori lililokamatwa likishusha mbao alfajiri ya tarehe 21,mwezi katika mji huo.

Ambapo mmiliki wake hajajitokeza hadi sasa. "Dereva wa lori hili lililokutwa na mbao 151 alikimbia, mmiliki wake hajatokea mpaka sasa," alisema Ngubiagai. Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi usalama ya wilaya hiyo alisema watu saba wanashikiliwa na jeshi la polisi kuhusiana na tukio hilo.

Aidha Ngubiagai aliwaonya viongozi wanaoshirikiana na wahalifu kutekeleza nakufanikisha uhalifu waache tabia hiyo mara moja. Alisema katika wilaya hiyo kunamtandao mkubwa unaowahusisha baadhi ya viongozi wa umma ambao sio waadilifu ambao umeamua kupambana na serikali. "Baada ya kuona nguvu kubwa zinatumika kudhibiti uvuvi haramu, wameamua kukimbilia kwenye mbao. Nawaambia hata huku tupo natutaendelea kuwashgulikia kikamilifu, kazi ndiokwanza imeanza hii," alitahadharisha.

Kuhusu viongozi wasio waadilifu, Ngubiagai alisema wapo katika ngazi zote za utawala katika wilaya hiyo. Hali ambayo ilikuwa inasababisha ugumu wa kuwatia mikononi wahalifu. Kutokana na taarifa  za misako na mbinu za kuwakamata kuvujishwa mapema na viongozi hao.

Hata hivyo dawa yao imeshapatikana na wanaendelea kukamatwa kinyume cha matarajio yao. Ametoa wito kwa viongozi na wananchi kuwa wazalendo nakushirikiana na wenye nia njema ya kukomesha uhalifu wilayani humo. Kwasababu jukumu hilo nilakila mmoja.