Wazanzibar wengi wanasubiri kwa hamu uteuzi wa timu ya Taifa ya Soka ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ ambapo wadau wengi wanaamini Zanzibar ina vipaji vingi sana ambavyo vitaleta upinzani mkubwa katika timu hiyo.
Lakini moja ya sifa za kuwa mchezaji wa timu ya Taifa ya Zanzibar ni kuwa na passport ambayo imetolewa na ofisi ya uhamiaji ya Zanzibar kwa na sio passport zilizotengenezwa Tanzania bara.
Kwa mujibu wa Afisa habari wa ZFA Ali Bakar ‘Cheupe’ amesema kuwa wachezaji watakaoitumikia timu ya Taifa ya Zanzibar ni kwa wale ambao Pasipoti zao zimetengenezwa visiwani Zanzibar.
“Wachezaji ambao wana sifa ya kuichezea Zanzibar Heroes ni wale ambao Pasipoti zao wamezipata Zanzibar, yani Pasipoti yake imetolewa hapa hapa Zanzibar,” alisema Cheupe.
Kwa maana hiyo, wachezaji wote wa Zanzibar ambao Passport zao zimetengenezwa Tanzania bara hawatakuwa na sifa ya kuitumikia Zanzibar Heroes.
Machi 16, 2017 ilikuwa ni siku nzuri na yenye historia kubwa kwa Zanzibar baada ya kuingizwa rasmi kuwa mwanachama wa 55 wa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ kufuatia Kikao cha 39 cha Mkutano Mkuu wa Shirikisho hilo kilichofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia baada ya kukubaliwa kwa kura 51 kati ya 54 zilizopigwa na nchi wanachama wa CAF.