F Makonda, Sirro wapishana Kauli | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Makonda, Sirro wapishana Kauli


Msanii wa hip hop Roma Mkatoliki alikamatwa April 5 usiku ambapo taarifa zilianza kuenea katika mitandao ya kijamii kuwa alikamatwa studio za Tongwe Records  na watu wasiojulikana akiwa na wenzake 4 na wakapelekwa  kusikojulikana.

Siku ya Ijumaa ya  April 7, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda, aliahidi Roma Mkatoliki, Moni pamoja na wengine wawili watapatikana Jumapili hii baada ya wasanii hao kutekwa na watu wasiojulikana Jumatano hii wakiwa Tongwe Record.

Alisema hayo akiwa nyumbani kwake Masaki jijini Dar es salaam, muda mchache baada ya kutembelewa na wasanii ambao walimtaka mkuu huyo kuwasaidia kupatikana kwa wasanii hao.

Akiongea na waandishi mbele ya wasanii hao, RC Makonda alisema kila mtanzania ana nafasi ya kumtafuta Roma na wenzake kwa kuwa hakuna anayejua watu hao wako wapi.

Mapema jana asubuhi kuhusu kutekwa kwa msanii huyo na wenzake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alisema kuwa hawezi kusema ni lini wasanii hao watapatikana kwani ni hadi pale upelelezi wanaouendesha utakapokamilika.

Sirro alikuwa akijibu swali la mwandishi wa habari aliyekuwa akiuliza kuhusu lini wasanii watapatikana kufuatia kauli ya Mkuu wa Mkoa aliyoitoa jana kuwa hadi Jumapili wasanii hao watakuwa wamepatikana.

“Mimi ni Kamishna wa Polisi siwezi kusema wasanii watapatikana lini, kama kuna kiongozi alitaja siku watakayopatikana, muulizeni yeye Alisema Sirro

Mara baada ya tamko la Kamanda wa Polisi na Kabla ya Siku ya Ijumapili (Leo), Wakina Roma waliripotiwa kuonekana kituo cha Polisi cha OysterBay jijini humo.