F Simba yapinga Banda kusimamishwa | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Simba yapinga Banda kusimamishwa

MAKAMU RAIS WA KLABU YA SIMBA, GEOFREY NYANGE 'KABURU' .

KLABU ya Simba imepinga hukumu ya kusimamishwa iliyotolewa kwa beki wao, Abdi Banda kwa kile ilichoeleza kuwa imetolewa na kamati isiyostahili, imeelezwa.

Banda amesimamishwa na Kamati ya Saa 72 ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi huku akisubiri suala lake la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla kuamuliwa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu Rais wa Klabu ya Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema hawakubaliani na uamuzi huo kwa sababu umetolewa na kamati isiyostahili.

"Ukiangalia kanuni zetu, tukio la Banda linaweza kukatiwa rufaa kwa sababu ni la uwanjani, hakukuwa na adhabu iliyotolewa pale, lakini liliripotiwa na kamisaa wa mchezo na kuonekana kwenye picha za video, hivyo waliopaswa kusikiliza ni chombo cha juu zaidi na sio Kamati ya Saa 72," alisema Kaburu.

Kiongozi huyo alisema wanapinga uamuzi huo kwa sababu Banda hakupata nafasi ya kusikilizwa kama ilivyo kwa mujibu wa kanuni na asili ya kosa lenyewe.

"Kuna wachezaji kadhaa huko nyuma waliwahi kufanya kosa kama hilo, lakini hawakuadhibiwa kama hivi, mfano mzuri ni kitendo kilichofanywa na Donald Ngoma, Amissi Tambwe na wengine ambao tuliripoti makosa yao, lakini mpaka sasa ni zaidi ya miaka miwili, ila kesi hizo hazijawahi kusikilizwa," Kaburu alisema.

Aliongeza kuwa Simba inaiomba TFF kusikiliza mapema kesi hiyo ili klabu ifahamu hatima ya kumtumia mchezi huyo katika mechi zinazofuata na pia kukaa bila kucheza kutashusha kiwango chake na itakuwa hasara kwa klabu na Timu ya Taifa, Taifa Stars.