Dodoma. Wabunge wa Kambi Rasimi ya Upinzani wamelaani shambulizi la mkutano wa viongozi wa CUF upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif na waandishi wa habari na kuitaka Serikali kuhakikisha matukio ya namna hiyo yanakomeshwa.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge ha leo Jumapili, naibu mnadhimu wa kambi hiyo, Ali Salehe amesema haiwezekani tukio kama la jana jijini Dar es Salaam likatokea katika nchi inayojali utawala wa sheria na uhuru wa kujieleza.
Salehe aliyeambatana na wabunge wengine wanane, amesema inashangaza kuona matukio ya watu kuvamia mkutano wakiwa na bastola hata baada ya tukio kama hilo kumtokea aliyekuwa Waziri wa Habari, Nape Nnauye.
Amemtaka Waziri wa Habari, Dk Harrison Mwakyembe na mwenzake wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kujitokeza na kutoa tamko na vitendo kukomesha matukio hayo.