Dar es Salaam. Baadhi ya wasomi wameijadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na kuitaka Serikali iwajibike kushughulikia yaliyotajwa.
Akizungumzia ripoti hiyo, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha alisema alitarajia kuona deni la Taifa lingekuwa limepungua, badala yake hivi sasa kuna hofu kwamba linaweza kuongezeka iwapo hautakuwapo udhibiti.
“Mikopo pia imeongezeka, ukiangalia ununuzi wa ndege japo wamesema wamelipa fedha taslimu, hizo wamezitoa wapi? Lakini sio mbaya ilimradi tusifikie hatua ya kutokopesheka,” amesema msomi huyo.
Mhadhiri wa Chuo cha Ualimu cha Duce, Dk Perpetua Urio amedai kuwa miradi mingi inayotekelezwa inagharimu kiasi kikubwa cha fedha huku ikiwa na tija ndogo kwa wananchi wenye kipato cha chini.
“Ukiangalia uchumi, tunazalisha nini kinachotuwezesha kulipa madeni? Ajira zilisimamishwa kwa zaidi ya miaka miwili, mzunguko wa pesa na biashara haupo vizuri, watu wanaumia,” amesema Dk Urio.
Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana amesema kuna watendaji wapiga dili wanaozalishwa na watumishi wa Serikali kwa kuwaingiza kinyemela na kushauri kuimarisha mifumo ya utunzaji taarifa kupitia kompyuta.
“Tunahitaji kufanya kazi ya ziada, huu ni uzembe wa baadhi ya watendaji na waliopo wawajibishwe,” amesema.
Akizungumza bungeni mjini Dodoma, Profesa Assad alisema juzi kuwa kati ya mapendekezo 102 ya Serikali Kuu, mapendekezo 29 ndiyo yametekelezwa huku katika Serikali za Mitaa ikiwa ni mapendezo matatu kati 79.
Profesa Assad alisema uchambuzi unaonyesha mapendekezo 511 kati ya 1,285 ya mradi wa maendeleo ya sekta ya kilimo ambayo ni sawa na asilimia 40 bado hayajatekelezwa.
Pia, alisema mapendekezo 742 kati ya 1,896 ya Mfuko wa Barabara ambayo ni sawa na asilimia 39 hayajatekelezwa.