Wapiga kura nchini Korea Kusini wamemchagua Moon Jae-in kuwa rais mpya wa taifa hilo, utafiti wa baada ya uchaguzi unaonesha.
Makadirio yanaonesha Bw Moon alipata 41.4% ya kura, mpinzani wake wa karibu mhafidhina Hong Joon-Pyo, akiwa na 23.3%.
Bw Moon amekuwa akiunga mkono kufanyika kwa mazungumzo na Korea Kaskazini, jambo ambalo litabadilisha sera ya sasa ya Korea Kusini.
Uchaguzi huo wa mapema uliitishwa baada ya Park Geun-hye kuondolewa madarakani kutokana na tuhuma za ufisadi.
Bi Park alidaiwa kumruhusu rafiki yake wa karibu kuitisha pesa kutoka kwa kampuni mbalimbali kwa kutumia jina lake, tuhuma ambazo amezikanusha.
Iwapo Bw Moon atathibitishwa kwua mshindi, huenda akaapishwa Jumatano.
Utafiti wa baada ya uchaguzi ulifanywa kwa pamoja na vituo vitatu vya runinga nchini humo.
Moon ni nani?
Ni mwana wa wakimbizi waliotoka Korea Kaskazini.
Bw Moon alifungwa jela alipokuwa mwanafunzi miaka ya 1970 kwa kuongoza maandamano dhidi ya kiongozi wa zamani wa kijeshi Park Chung-hee - babake Bi Park.
Baadaye alihudumu katika vikosi maalum vya wanajeshi wa Korea Kusini kabla ya kuwa wakili wa haki za kibinadamu.
Bw Moon, ambaye chama chake cha Democratic Party ni cha mrengo wa kati-kushoto, aliwania urais dhidi ya Bi Park mwaka 2012 lakini akashindwa.
Alijipigia debe kama mtu ambaye anaweza kusongeza taifa hilo mbele kutoka kipindi cha misukosuko na kashfa chini ya Bi Park.
"Nahisi kwamba sio mimi pekee na chama change bali pia watu wenyewe wanataka serikali ya mabadiliko," alisema alipokuwa anapiga kura.
Sera zake?
Bw Moon amekuwa akiunga mkono kufanyika kwa mazungumzo na Korea kaskazini lakini kuendelee kwua na shinikizo na vikwazo dhidi ya utawala wa taifa hilo.
Hili ni kinyume na serikali ya Bi Park aliyekatiza karibu uhusiano wote na Korea Kaskazini.
Amekuwa akikosoa serikali mbili za awali kwa kushindwa kuzuia mradi wa Korea Kaskazini kustawisha silaha.
Lakini ingawa wasiwasi katika rasi ya Korea ulifanya uchaguzi huo kufuatiliwa kwa karibu, walichoangazia zaidi raia wa Korea Kusini ni kukomesha ufisadi na kuimarisha uchumi. Ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana umekithiri.
Bw Moon amezungumzia pia wazo la kufanyia mageuzi kampuni kubwa zinazomilikuwa na familia nchini humo, ambazo hutawala uzalishaji na uchumi.