Kikosi cha Yanga kinazidi kupukutika kwa baadhi ya nyota wa timu hiyo wanaonekana kuondoka ambapo sasa beki mgumu, Vincent Bossou raia wa Togo naye ametangaza nia ya kuondoka baada ya kugomea kusaini mkataba mpya huku uongozi ukimpa mkono wa kwaheri.
Bossou amegoma kusaini mkataba mpya wa kuendelea kukipiga ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Mzambia, George Lwandamina baada ya mkataba wake wa awali wa miaka miwili kufika ukingoni hivi karibuni.
Hii inakuja siku chache baada ya beki huyo kuliambia gazeti la Championi kuwa yupo tayari kusaini mkataba Simba, ikiwa viongozi wa klabu hiyo watamtafuta wakiwa na ofa nono.
Katibu wa Yanga, Boniface Mkwasa amesema wameachana na beki huyo aliyewasaidia kutwaa mataji mawili ya ligi kuu mfululizo kutokana na yeye kushindwa kusaini mkataba mpya ambao ungemuweka kikosini hapo licha ya kufanya jitihada za kumbakiza.
“Rasmi sasa Bossou (Vincent) hatakuwa sehemu yetu kwenye msimu ujao wa ligi baada ya kuamua kuondoka punde tu mkataba wake ulipofika ukingoni hivi karibuni, hivyo kumfanya awe mchezaji huru ambaye anaweza kwenda kokote kule.
“Sisi kwa upande wetu tulipanga kuwa naye na tulifanya kila jitihada tukiwa na lengo la kumbakiza lakini yeye ameona vyema kwenda sehemu nyingine na hatuna njia nyingine ya kumzuia kuondoka kwa sababu alishaamua kufanya hivyo,” alisema Mkwasa.