WATU watatu wameuawa kikatili kwa kuchinjwa katika matukio tofauti yalitokea mkoani Rukwa, mmoja kati yao akiwa ni mfanyabiashara kutoka jijini Mbeya, Elizabeth Kalenga (36).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alithibitisha mauaji hayo akisema yalitokea Juni 6, mwaka huu saa 3:45 usiku katika Kijiji cha Sakalilo kilichopo katika Bonde la Ziwa Rukwa, Kata ya Ilemba wilayani Sumbawanga.
Alisema kabla ya kuuawa, wauaji walimvunja Elizabeth taya la kushoto walipomvamia. “Chanzo cha mauaji hayo ya kikatili bado kinachunguzwa,” alisisitiza Kamanda Kyando . “Watuhumiwa walimkuta marehemu akiwa nje ya nyumba yake na kumuuliza kama mtoto wake wa kiume ambaye ni Justine Kalenga yupo na alipowauliza wa nini, ndipo walipofyatua risasi moja juu na kumpiga na kumvamia,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamanda Kyando watuhumiwa wawili ambao hakuwa tayari kuwataja majina yao wamekamatwa kwa mahojiano zaidi na watafikishwa mahakamani pindi upelelezi wa awali wa kipolisi utakapokamilika.
Katika tukio lingine; watu wawili mmoja akijulikana kwa jina moja la Rasi wameuawa kwa kushambuliwa na kuchinjwa kisha miili yao kuchomwa na kuteketezwa kwa moto katika Kijiji cha Mpui kilichopo katika Wilaya ya Sumbawanga wakituhumiwa kwa wizi wa mifugo.
Kamanda Kyando alisema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 14 mwaka huu mchana katika kijiji cha Mpui, Kata na tarafa ya Mpui wilayani Sumbawanga. “Chanzo cha mauaji hayo ni wizi wa mifugo ambapo wawili hao walihisiwa kuwa ni wezi, ambapo walibambwa na wananchi wenye hasira wakiwa wanaswaga ng’ombe wawili wa wizi,” alisema.
Katika tukio lingine Mkazi wa Mtaa wa Kashai katika Manispaa ya Sumbawanga, John Chinga (29) alikutwa akimiliki risasi mbili za bunduki aina ya shotgun bila kuwa na vibali halali. Kamanda Kyando alisema mtuhumiwa huyo ambaye amekamatwa kwa mahojiano alikutwa akiwa na risasi hizo chumbani kwake katika Mtaa wa Kashai katika Manispaa ya Sumbawanga. Alisema mkasa huo ulitokea Juni 13 mwaka huu saa 3:5o usiku