Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipozindua Kamusi Kuu ya Kiswahili kwenye ukumbi wa Bunge Mjini Dodoma Juni 19, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha Kamusi Kuu ya Kiswahili baada ya kuizindua kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma Juni 19, 2017. Kulia ni Mwenyekiti wa Bunge na Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu. Kushoto ni Balozi wa Kiswahili Afrika, Mama Salma Kikwete. Wapili kushoto ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa Taifa na katika kulinda umoja wa Kitaifa.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatatu, Juni 19, 2017) wakati akizungumza na wabunge, viongozi wa Serikali na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili uliofanyika kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.
“Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa nchi yetu na katika kulinda umoja wa Kitaifa. Hakika lugha ya Kiswahili ndiyo inayotufanya tuwe Watanzania. Hivyo, tunaithamini sana na kwetu hii ni lulu na tunu ya Taifa,” amesema.
Waziri Mkuu amesema uzinduzi wa Kamusi hiyo unaenda sambamba na azma ya Serikali ya kutumia Kiswahili kwenye shughuli zote za kitaifa kama vile mikutano, mijadala, semina na ufundishaji shuleni.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhimiza matumizi ya Kiswahili kwenye mikutano na matukio muhimu ya kitaifa, kama vile dhifa za kitaifa anazowaandalia wageni wake kutoka nje ya nchi.
“Hata alipokuwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika wa mwaka 2017, Mheshimiwa Rais alitumia Kiswahili kuhutubia mkutano huo. Amekuwa akifanya hivyo, hata kwenye mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo lake ni kuitangaza lugha hii ya Kiswahili,” alisema.
Aliwasihi wazazi kote nchini wahakikishe kuwa watoto wao wanapata kamusi hiyo kama moja ya nyenzo zao za kujifunza lugha ya Kiswahili. “Vilevile, ninashauri, makundi mengine kama vile waheshimiwa wabunge, wanahabari, wakalimani, wafasiri, waandishi na wahariri wa vitabu, maofisa mawasiliano wa kwenye ofisi zetu, muone umuhimu wa kununua Kamusi hii, ili iwasaidie kujiimarisha kwenye matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu,” aliongeza.
Mapema, akizungumza katika hafla hiyo fupi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe alisema Kiswahili ni lugha ya pili inayotumiwa na watu wengi zaidi barani Afrika lakini pia ni lugha ya 10 kati ya lugha 6,000 zinazozungumzwa na watu wengi duniani.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Dk. Seleman Sewangi alisema kazi ya kuandaa kamusi hiyo ilianza Agosti 12, 2011 na kukamilika mwaka 2015 ambapo toleo la kwanza lilichapishwa.
Alisema kamusi hiyo imekusanya maneno mengi makuu (vidahizo) kuliko kamusi zilizotangulia na kwamba ya sasa ina maneno hayo 45,500.