F DCI awaanika vigogo wapya kwenda Keko | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

DCI awaanika vigogo wapya kwenda Keko

WAKATI kasi ya kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa makosa mbalimbali yanayohusiana na rushwa na ufisadi ikionekana kuwa ya juu katika kipindi cha wiki mbili zilizopita,-

imebainika kuwa mwenendo huo wa kuwafikisha wahusika mbele ya mkono wa sheria utaendelea zaidi kutokana na uchunguzi mkali unaohusisha vigogo wa zaidi ya maeneo 10.

Hali hiyo imebainika kutokana na taarifa ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, aliyefichua kuwa wako katika hatua nzuri za uchunguzi dhidi ya watuhumiwa wa masuala mbalimbali.

Boaz alisema kutokana na uchunguzi wao huo, wanaendelea kufikisha majalada ya wahusika kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambaye ndiye huwafikisha wahusika mahakamani pindi ikionekana inafaa na kwamba miongoni mwa wale wanaokamilisha uchunguzi ni pamoja na wa mashtaka ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.

Kwa kawaida, DCI hawafikishi mahakamani watuhumiwa, bali uchunguzi wake katika masuala yanayohusiana na jinai, ndiyo hufanikisha sheria kuchukua mkondo wake kupitia mchakato unaohusisha DPP na mahakama ambayo ndiyo hutoa uamuzi .

Hivi karibuni, watu wanaoshikilia nafasi za uongozi katika taasisi mbalimbali na wafanyabiashara wakubwa, walifikishwa mfululizo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kukabiliana na tuhuma mbalimbali na wengi wao kujikuta wakikosa dhamana kutokana na aina ya makosa yanayowakabili, hivyo kupelekwa katika mahabusu ya Gereza la Keko jijini Dar es Salaam.

Mashtaka yatokanayo na tuhuma zinazohusiana na uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ndiyo yaliyowaponza wale waliofikishwa mahakamani hivi karibuni na kujikuta wakiishia kupelekwa Keko.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Nipashe jana, DCI Boaz alisema wako katika hatua nzuri za uchunguzi wa baadhi ya masuala zaidi ya 10 yaliyo mikononi mwao na kwamba, kwa sababu hiyo, kuna watu wazito watakaofikishwa mahakamani wakati wowote ikiwa DPP ataona inafaa kutokana na makosa mbalimbali yakiwamo ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.

Akieleza zaidi, DCI Boaz alisisisitiza kuwa hivi sasa, ofisi yake ina masuala mengi mazito ya kiuchunguzi na wanaendelea na uchunguzi kwa umakini mkubwa ili kuepuka kasoro zinazoweza kuiingizia serikali hasara.

“Kesi ni nyingi sana na zote zinahitaji upepelezi uliojaa umakini wa hali ya juu. Hatutaki kukurupuka, ila zipo kesi ambazo majalada yake wakati wowote kuanzia sasa yatakabidhiwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DPP) kwa hatua nyingine,” alisema.

Bila kutaja majina ya wahusika, DCI Boaz alisema miongoni mwa uchunguzi mkubwa wanaoendelea kuukamilisha na kesi zake kuwa mbioni kufikishwa kwa DPP ili hatimaye watuhumiwa wapandishwe kizimbani itakapobidi kuwa ni pamoja na zile za ubadhirifu bandarini, uhujumu uchumi, zinazohusu ujangili na nyara za serikali, dawa za kulevya, utapeli, usafirishwaji wa mchanga wa madini (makinikia) kwenda nje na nyinginezo nyingi.

“Ninaposema kesi ni nyingi, ni nyingi kwelikweli. Hizo nilizotaja ni baadhi tu, lakini tuna kesi nyingi na nyingine majalada ya kesi zake tumekuwa tukiyapeleka kwa DPP…yeye (DPP) anaposoma na kuona bado zinahitaji kuongezewa mambo, huturudishia kwa ajili ya kufanya hivyo,” alifafanua DCI na kuongeza:

“Unajua upelelezi huwa siyo wa siku moja bali ni endelevu. Na kesi tulizonazo zinahitaji umakini mkubwa.”

UCHUNGUZI MAKINIKIA
Akifafanua kuhusu uchunguzi wao kuhusiana na sakata la makinikia lililoibuliwa hivi karibuni baada ya kamati mbili zilizoundwa na Rais John Magufuli kuonyesha kuwa kuna upotevu mkubwa wa mapato yaliyotokana na hujuma za baadhi ya maofisa wa juu wa serikali, DCI Boaz alisema wapo katika mchakato wa kukamilisha upelelezi ili jalada lake likabidhiwe kwa DPP na kisha mchakato wa kuwapeleka wahusika mahakamani kuendelea.

Alisema katika suala hilo, kama ilivyo kwenye uchunguzi wao wa masuala mengine, hakuna kinachoangaliwa bali ni kuzingatia sheria za nchi, huku wahusika wakichukuliwa hatua stahili bila kujali umaarufu, sura wala nafasi ya mtuhumiwa katika jamii.

“Kama wewe ulikuwa hujanaswa na ulifanya uhalifu wa namna yoyote ile, hatutakuacha… wewe ni mhalifu. Hapa hatuangalii umaarufu wa watu. (Bali) tunaangalia je, wewe ni mhalifu?”alisema Boaz.