F Kanisa Anglikana kubadilisha Katiba yake | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kanisa Anglikana kubadilisha Katiba yake

Kanisa Anglikana Tanzania linakusudia kufanya mabadiliko ya katiba yake ili kuruhusu kanisa kufanya uwekezaji.

Akizungumza wakati wa ibada iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Albano jijini Dar es Salaam leo, Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini, Dk Jacob Chimeledya amesema lengo la mabadiliko hayo ni kulifanya kanisa kugusa maisha ya watu.

Dk Chimeledya amesema kanisa hilo linaunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kuwainua watu wa chini na kwamba, jambo hilo haliwezi kufanikiwa kama injili haitawafikia.

"Nguvu ya kanisa lazima iguse maisha ya watu wa chini. Tutafanya mabadiliko ya katiba ili kuruhusu uwekezaji ambao tulishaanza kuufanya," amesema Dk Chimeledya.

Askofu Chimeledya amewataka mapadri wa kanisa hilo kufanya jitihada za kuanzisha parokia zingine katika maeneo yao kwa sababu Dayosisi ya Dar es Salaam ina parokia chache ambazo hazifiki 100.