Dar es Salaam. Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ataendelea kusota rumande hadi Jumatatu baada ya taratibu za polisi za kiuchunguzi kutokamilika, licha ya saa 48 alizotakiwa kukaa mahabusu kumalizika.
Mdee, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), alikamatwa Julai 4 kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi na sasa atakaa mahabusu kwa saa 144.
Hapi aliagiza Mdee awekwe ndani kwa saa 48 kwa madai ya kutoa kauli za kichochezi dhidi ya Rais John Magufuli.
Agizo la saa 48 lililotolewa na Hapi lilikamilika juzi saa mbili usiku, lakini polisi wa kituo cha Oysterbay hawakumuachia mbunge huyo na kumfanya aendelee kukaa mpaka Jumatatu hivyo kufikisha saa 144.
Akizungumza jana na gazeti hili, Wakili Peter Kibatala alisema hawana jinsi badala yake wanaendelea kutii agizo la polisi la kwamba bado uchunguzi haujakamilika dhidi ya mteja wake ingawa kuna makosa mengi ya kisheria yamefanyika.
“Kibaya zaidi hii ishu imeangukia siku ya sikukuu na kesho ni wikiendi, Mahakama hazifanyi kazi. Lakini nina uhakika hadi Jumatatu tutapambana kisheria ili kuhakikisha mteja wangu anafikishwa mahakamani.
“Uzuri wenyewe mteja wangu ni mwanasheria, kwa hiyo ameshatupa maelekezo ya nini cha kufanya kisheria kuhusu mchakato wake wa kukamatwa na sheria za saa 48 zinavyotumiwa vibaya na baadhi ya wakuu wa mikoa na wa wilaya,” alisema Kibatala.
Kibatala alisema Mdee yupo katika hali nzuri kukanusha madai kwamba amegoma kula kama ilivyoandikwa na baadhi ya magazeti. Alisema Mdee alijiandaa kisaikolojia kuhusu mazingira ya polisi.
“Hii sheria ya saa 48, lazima tupambane nayo. Kwa sababu imeshaanza kuzoeleka, ilianza kwa Meya wa Arusha, ikaja kwa Meya wa Ubungo na madiwani wengine, sasa imekuja kwa mbunge wa kuchaguliwa na wananchi,” alisema Kibatala.
Alisema watakwenda mahakamani kwa hatua zaidi kwani mteja wake ameshapitisha muda wa saa 48 alizotakiwa kukaa rumande kwa amri ya mkuu wa wilaya.
Mbali na Mdee, viongozi wengine wa Chadema waliowahi kukumbwa na kadhia hiyo ni Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ambaye aliwekwa ndani saa 48 kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori.
Jacob ambaye pia ni diwani wa Ubungo aliwekwa ndani kwa amri hiyo kwa madai ya kufanya mkutano na viongozi wa Chadema katika ukumbi wa manispaa hiyo kinyume cha sheria.
Lakini, kwa Jacob ilikuwa tofauti baada ya saa hizo kwisha aliachiwa na hapakuwa na taarifa za kufikishwa mahakamani kama sheria inavyotaka.
Mwingine ni Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ambaye inadaiwa alikamatwa kwa amri ya mkuu wa mkoa huo, Mrisho Gambo akiwa na madiwani wawili wa Chadema na kukaa mahabusu kwa saa 48.
Walikamatwa walipokwenda katika Shule ya Mtakatifu Lucky Vincent kutoa rambirambi kwa viongozi wa shule hiyo kutokana na ajali mbaya iliyoua dereva, walimu wawili na wanafunzi 33.