F Mwengine auwawa Kibiti usiku wa kuamkia leo | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mwengine auwawa Kibiti usiku wa kuamkia leo



Mkazi mmoja wa kitongoji cha Nyambwanda kilichopo katika Kijiji cha Hanga wilayani Kibiti aliyetambulika kwa jina la Hamis Ndikanye (54) ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo Jumamosi akiwa nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa maelezo ya ndugu wa marehemu alijitambulisha kwa jina la Hamis Saidi amesema watu kama watano wakiwa na bunduki walifika nyumbani kwa ndugu yake saa 6 usiku, kisha kufanya mauaji hayo.

Alisema kabla ya kufanya mauaji hayo walimfunga mke wa marehemu kitambaa usoni na kisha kumpiga risasi mbili mume wake.

Mganga wa Kituo cha Afya Kibiti Dk Sadock Bandiko amesema Ndikaye amepigwa risasi mbili mwilini mwake, moja kichwani na nyingine mgongoni.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi wa Rufiji, Onesmo Lyanga, amesema polisi wamekwenda eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi.