Rahim Kwangaya, mkazi wa Mandela, Ikwiriri mkoani Rufiji, ameuawa kwa kupigwa riasi na watu wasiofahamika, kisha maiti yake kwenda kutupwa kwenye jalala lililopo kando ya nyumba yake, tukio lililotokea usiku wa kuamkia juzi.
Katika tukio hilo, mke wa marehemu, Tatu Mnete, naye alipigwa risasi kwenye titi la kushoto ambapo alikimbizwa hospitali anakoendelea na matibabu.
Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Ikwiriri, Dkt. Iddy Malinda, alithibitisha kupokea mwili wa Kwangaya, ukiwa na majeraha mawili ya risasi, tumboni na kwenye bega ambapo alieleza kwamba baada ya kuufanyia uchunguzi mwili huo, waligundua pia kwamba ulikuwa na michubuko kichwani, jambo linaloonesha maiti iliburuzwa baada ya mauaji.
Akaongeza kwamba walimpokea pia mke wa marehemu aliyekuwa amepigwa risasi kwenye ziwa, na kwamba alihamishiwa Hospitali ya Mchukwi kwa matibabu zaidi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji, Onesmo Lyanga, alipotafutwa ili kuthibitisha tukio hilo, alisema hawezi kujibu chochote kwa sababu hakuwepo ofisini.
Kwa mujibu wa mashuhuda, wauaji hao walifika nyumbani kwa Kwanganya anayejishughulisha na biashara maeneo ya Mnadani, ambapo walimuamuru kufungua mlango na alipofanya hivyo tu, alipigwa risasi na kufa papo hapo.