F Serikali yanusa ufisadi mwingine | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Serikali yanusa ufisadi mwingine

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imesema itatuma timu maalum wiki ijayo kwenda kufanya uchunguzi wa haraka kutokana na kuwapo harufu ya ubadhirifu katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo, alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Rose Kamili.

Kamili alitaka kujua kigezo gani kimetumika kuwaacha watumishi waliofanya ubadhirifu kwenye halmashauri hiyo kuendelea kuwa kazini.

Akijibu swali hilo, Jafo alisema wizi ni wizi hakuna mdogo wala mkubwa na kwamba katika Halmashauri hiyo inaonekana kuna madudu makubwa.

“Ofisi yetu itatuma timu maalum wiki ijayo kwenda kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini matatizo hayo,” alisema Jafo

Katika swali la msingi, Kamili alisema serikali ina utaratibu wa kutoa fedha kwa ajili ya shule za bweni nchini na kuanzia Agosti 2013 na Februari 2014, halmashauri hiyo ilipokea Sh. milioni 508.77 kwa ajili ya chakula shule za bweni.

“Taarifa zinaonyesha kuwa fedha zilizotumika kununua chakula ni Sh. milioni 225.5 kwa takwimu hizo bakio ni Sh.milioni 283.1 na kwa mujibu wa mkaguzi bakaa hiyo haionekani kwenye akaunti yoyote ya benki,”alisema Kamili.

Alihoji fedha hizo zimerudishwa Hazina bila uwapo wa nyaraka zozote toka halmashauri kuonesha muamala unavyofanya kazi.

Akijibu swali hilo, Jafo alisema halmashauri hiyo ilipokea fedha hizo kwa ajili ya shule nne na kwamba bakaa hizo hazikurudishwa Hazina badala yake zilibadilishwa matumizi kwa kuombewa kibali kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Alisema kamati ya fedha na mipango ya halmashauri ilipokea taarifa ya matumizi ya fedha na iliagiza fedha hizo zirudishwe kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza shughuli za ununuzi wa vifaa na samani kwa wanafunzi wa shule husika.

Alibainisha kiasi cha Sh.Milioni 130 zimepelekwa kwenye akaunti za vijiji vya Gendabi, Bassodesh, Katesh na Balangdalalu kwa ajili ya kununulia magodoro, vitanda na ukarabati wa mabweni kwa shule za msingi za bweni.

“Halmashauri imeagizwa kurejesha fedha zilizobaki kiasi cha Sh. milioni 153.1 ndani ya mwaka huu wa fedha,” alisema.

Hata hivyo alisema kutokana na matumizi ya fedha za halmashauri yasiyoridhisha ikiwa ni pamoja na matumizi ya fedha hzo tangu Aprili, mwaka jana, Mkurugenzi Mtendaji amesimamishwa kazi na mamlaka yake ya nidhamu sambamba na ofisa mipango wa wilaya, mweka hazina na wahasibu wawili waliosimamishwa na Baraza la Madiwani ili kupisha uchunguzi.