F Umeipata hii ya Ajira kumwagwa? | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Umeipata hii ya Ajira kumwagwa?


SERIKALI inatarajia kutoa vibali 3,000 vya ajira katika sekta ya afya, zikihusisha madaktari na wauguzi kwa ajili ya vituo vya afya vya kata ili kuboresha sekta hiyo, imeelezwa hapa jana.

Pia serikali imetangaza kuwa itatoa vibali vya ajira za maofisa hesabu 535 kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati nchini ili kushughulikia ipasavyo ukusanyaji wa mapato.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro, ndiye aliyetangaza neema hiyo kwa wasomi wanaosubiri ajira serikalini wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhusu maadili na uwajibikaji mahali pa kazi.

Alisema vibali vya ajira hizo vitatolewa wiki ijayo huku akiwataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu ili kujenga utumishi wa umma wenye uadilifu.

"Naomba wanaoharibu wasihamishwe na kupelekwa maeneo mengine, wakifanya hivyo watakuwa wanaharibu utumishi wa umma, ufumbuzi ni kuchukua hatua palepale alipo," alisema Dk. Ndumbaro.

Aliongeza kuwa sekta zinatakiwa kujenga utamaduni wa kuwapongeza watumishi wa umma wanaofanya vizuri kwenye maeneo yao ya kazi ili wajitume zaidi na kuhamasisha wengine.

Katika kikao kazi hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Eliakim Maswi, alisema vituo vingi vya afya vimefungwa kutokana na watumishi kuwa na vyeti vya kughushi hivyo vingi havina watumishi.

Alisema uhakiki wa vyeti feki bado haujamalizika, lakini akasisitiza kuwa ni muhimu kwa sasa serikali kutoa vibali vya ajira mpya kwa kuwa watumishi waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi ni wengi hivyo kuna haja ya kuziba pengo hilo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya alisema serikali itaendelea kuajiri watumishi katika sekta ya afya.

Katika ufafanuzi kuhusu ajira mpya zitakazotolewa wiki ijayo, Dk. Ulisubisya alisema kila mkoa utapata mgawo wa wataalamu hao watakaoungana na madaktari 258 ambao walisailiwa kwa ajili ya kwenda kufanya kazi Kenya, lakini baadaye wakaajiriwa nchini.

Katika mwaka huu wa fedha, serikali imeahidi kutoa vibali vya ajira za moja kwa moja 52,436 katika sekta zake mbalimbali.

Aprili 19, kufuatia Mahakama ya Kenya kutoondoa pingamizi lililofunguliwa dhidi ya ajira za madaktari kutoka nchini walioombwa huko, Rais John Magufuli aliamua wataalamu 258 waliokuwa wamejitokeza kuchangamkia fursa hiyo waajiriwe na serikali.

Madaktari hao ndiyo waliokidhi vigezo vilivyotakiwa kwenda kufanya kazi nchini Kenya kati ya 496 waliokuwa wameomba.

Machi 18, ujumbe wa serikali ya Kenya ukiongozwa na Waziri wa Afya nchini humo, Dk. Cleopa Mailu ulikutana na Rais Magufuli na kuomba kuajiri kwa mkataba madaktari 500 ili kupunguza uhaba wa wataalamu hao wa afya uliotokana na mgomo nchini humo.

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Muhammad Kambi alipapata kusema idadi ya madaktari wanaohitajika nchini ni 3,510 na katika idadi hiyo, mahitaji zaidi yapo kwenye hospitali za wilaya kunakokosekana madaktari 832, za rufani (460), vituo vya afya (816), Bugando (152) na Hospitali ya Taifa Muhimbili madaktari 235.

Nyingine ni KCMC (143), hospitali za rufani za mikoa (460), madaktari 111 katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Hospitali ya Ocean Road (57), Mirembe (37), CCBRT (26) na Rufani Mbeya (106).

Mei 3, Waziri Kivuli wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Godwin Mollel aliliambia Bunge kuwa uwiano kati ya madaktari na wagonjwa nchini kwa sasa si mzuri.

Akinukuu ripoti ya Madaktari Wenza wa Afrika (Africa Cuamm) ya mwaka jana, Dk. Mollel alisema asilimia 74 ya madaktari wanaishi mjini na daktari mmoja anahudumia wagonjwa 78,880 kwa maeneo ya vijijini, kinyume cha maelekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) linalotaka daktari mmoja ahudumie wagonjwa elfu moja (1:1,000).

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa Oktoba 2016, Tanzania ina upungufu wa asilimia 58.1 ya madaktari bingwa, wauguzi wa sekta ya umma II kwa asilimia 54.4, wataalamu wa miale kwa asilimia 50.8 na maofisa kliniki kwa asilimia 50.

Pia kuna upungufu wa madaktari wasaidizi na madaktari wasaidizi wa meno kwa asilimia 46.2, wafamasia kwa asilimia 49.9, mabwana afya kwa asilimia 45.7, mafundi sanifu wa maabara kwa asilimia 41.5, maofisa kliniki wasaidizi kwa asilimia 40.7 na madaktari kwa asilimia 37.3.

Wakati serikali ikishindwa kuajiri madaktari, Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Obadia Nyongela, aliiambia Nipashe mwishoni mwa mwaka jana kuwa kuna madaktari 1,700 mtaani ambao wana sifa, lakini hawajaajiriwa.

"Kama mwaka huu (2016) utaisha bila vibali vya ajira kutoka, maana yake mpaka mwakani (2017) kutakuwa na madaktari 2,866 wasio na ajira licha ya kuwapo kwa upungufu wa wataalamu hao," alisema Dk. Nyongela.