MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala, amewaonya wanasiasa katika Jiji la Mbeya wanaowakatisha tamaa wananchi wanaojitolea kuchangia shughuli za maendeleo na kuwafananisha watu hao na joka la mdimu.
Makala aliyasema hayo jana alipokuwa akikabidhiwa jengo la darasa katika Shule ya Msingi Iyela, iliyoko jijini hapa ambalo limejengwa kwa kujitolea na Ndele Mwaselela.
Alitoa onyo hilo baada ya kupata taarifa kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wameshaanza kumpiga vita kijana huyo kutokana na misaada anayojitolea katika kuboresha sekta ya elimu kwa madai kuwa anaandaa mazingira ya kugombea nafasi zao kwenye uchaguzi ujao.
Makala alisema wanasiasa hao ni sawa na joka la mdimu ambalo halili machungwa wala malimao lakini hujificha kwenye mti wa matunda husika na kuwaondoa wanaokwenda kuchuma.
Alisema wanasiasa hao hawajishughulishi na utatuzi wa changamoto za wananchi ndiyo maana wanajishtukia.
“Kijana wa watu amejitolea kwa fedha zake kujenga jengo hili mpaka limekamilika, amenunua madawati na kuyaweka humu lakini anaanza kupigwa vita eti anatengeneza mazingira ya kugombea nafasi zao.
Huo ni ujinga uliopitiliza,” alisema Makala. Kwa upande wake, Mwanselela ambaye ni mzaliwa wa Iyela, alisema aliamua kujenga darasa hilo ili kupunguza kero ya upungufu wa madarasa katika shule hiyo ambayo yeye mwenyewe ni moja ya matunda yake.
Alisema licha ya kujenga darasa hilo pia ameajiri walinzi na kununua vifaa mbalimbali na kulipa gharama za umeme katika shule hiyo, gharama ambazo kwa pamoja zinagharimu Sh. milioni 40 kutoka mfukoni mwake.
Mwanselela alisema hana mpango wowote wa kugombea katika nafasi za kisiasa kwenye kata hiyo wala katika jimbo lakini ameamua kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha miundombinu ya elimu inaboreshwa.
Aliwataka wanaowaza masuala ya umaarufu wa kisiasa kumwacha aendelee kuchangia maendeleo ya elimu huku akiwahamasisha wasomi wengine kutoka katika kata hiyo wanaoishi maeneo mbalimbali nchini kujitokeza kwenda kuchangia maendeleo.