Maji ya bahari.
Kama hujaona basi kwa taarifa yako, bahari mbili za Atlantic na Pacific, kuna sehemu zinakutana lakini cha ajabu, maji yanaonekana ‘kutochanganyika’, upo mpaka kabisa katika maji, unaoyatofautisha maji ya bahari moja na bahari nyingine, ya upande mmoja yakionesha kuwa na rangi tofauti na ya upande wa pili.
Wengine wanalihusisha tukio hili na nguvu zisizoonekana, wengine wanaeleza ni miongoni mwa ishara kwamba Mungu yupo na wengine hawaelewi chochote. Lakini nini hasa kinachosababisha hali hii?
Kuweka mambo sawa, lazima ieleweke kwamba si kwamba maji ya bahari hizo mbili hayachanganyikani, isipokuwa huchukua muda fulani kuchanganyikana. Kwa sababu gani?
Pacific ndiyo bahari kubwa kuliko zote duniani, ikikusanya maji kutoka Antarctica mpaka Arctic, kuanzia ncha ya Kaskazini mpaka ncha ya Kusini ya dunia. Kwa kuwa sehemu kubwa ya vyanzo vya maji yake ni theluji, kiwango cha chumvi kwenye maji ya bahari hiyo, ni kidogo ukilinganisha na maji ya bahari ya Atlantic.
Kisayansi, maji yenye kiwango tofauti cha chumvi, huchukua muda mrefu kuchanganyikana, na ushahidi wa hili, inaelezwa kwamba eneo ambalo mto Amazon unaingiza maji baharini, kwa kuwa maji ya mto hayana chumvi tofauti na ya baharini, ukiwa umbali wa zaidi ya mita 200 baharini, usawa wa eneo hilo, kuna maji baridi yasiyo na chumvi kabisa.
Kwa hiyo, sababu ya kwanza ya kitaalamu ya maji hayo ‘kutochanganyikana’, ni tofauti ya kiwango cha chumvi kati ya bahari hizo mbili, Atlantic ikitajwa kuwa ndiyo yenye chumvi nyingi zaidi.
Sababu nyingine, inaelezwa kwamba kitaalamu, maji ya Bahari ya Atlantic, yanajongea kuelekea upande wa Kusini. Wakati huohuo, maji ya Pacific, yenyewe yanajongea kwa mfumo ambao kitaalamu huitwa circumpolar movement, yaani mwendo wa kuzunguka kutoka ncha moja ya dunia mpaka nyingine.
Kwa lugha nyepesi, maji ya Pacific, yanajongea kwa mfumo wa kuzunguka duara lakini yakitokea Mashariki. Mkondo wa Bahari ya Atlantic una nguvu zaidi kwa sababu una uelekeo mmoja, kwa hiyo katika eneo yanapokutana, maji ya Atlantic yanakuwa kwenye kasi tofauti inayokinzana na maji ya Pacific, kwa hiyo yanalazimika kusafiri kwenye mstari mmoja ulionyooka kwa umbali fulani kabla ya baadaye kuanza kuchanganyikana.
Sababu ya tatu, inaelezwa kwamba kasi ya maji ya juu ya bahari, ni tofauti na kasi ya maji ya chini ya bahari, kwa hiyo pale bahari hizo mbili zinapokutana, maji yanayoanza kuchanganyikana, huwa ni ya chini kwa sababu ya kasi yake kisha baadaye, ndiyo maji ya juu nayo huchanginyakana taratibu kwa sababu ya kasi yake.
Kwa hiyo, ile dhana kwamba bahari hizo mbili hazichanganyikani, si ya kweli kwa sababu kitaalamu imethibitika kwamba maji hayo huchanganyikana.