Ikiwa ni miezi minne tangu chama cha soka cha Zanzibar kipewe uanachama na CAF hii leo habari mpya kutoka CAF zinasema chama hicho kimevuliwa uanachama.
Raisi wa soka barani Afrka Caf Ahmad Said amesema Zanzibar walipewa uanachama kimakosa na kama sheria zingepitiwa vizuri wasingepewa uanachama.
“Walipewa uanachama bila kupitia vizuri kanuni ambazo ziko wazi na zinaeleza kila kitu, kama kanuni na sheria zingepitiwa kiufasaha wasingepewa uanachama”
Sababu kubwa ambayo CAF wameivua uanachama Zanzibar ni kutokana na kisiwa hicho kuwa ndani ya Tanzania ambao nao ni wanachama wa CAF.
“Jina la nchi linatokana na jina linaloandikwa katika umoja wa mataifa UN na Zanzibar katika umoja huo inafahamika ipo ndani ya nchi iitwayo Tanzania ambao ni wanachama wa CAF” aliendelea kusema Rais Ahmad.
Hilo ni pigo kubwa kwa Wazanzibar kwani wakati huu walikuwa wakipambana kupata uanachama wa FIFA ambao wameukosa na wa CAF nao pia wamekosa.
Kwa maana hiyo ndoto ya kisiwa cha Zanzibar kushiriki michuano ya CAF kama mwanachama zimekufa rasmi na sasa watakuwa wakishiriki michuano hiyo kama Tanzania(Zanzibar na Tanzania bara).