Dar es Salaam. Nyumba za kifahari zilizojengwa pembezoni mwa Barabara ya Morogoro kuanzia maeneo ya Kimara mpaka Kiluvya jijini Dar es Salaam zimekumbwa na bomoabomoa ya aina yake.
Pengine hilo linafahamika na wengi, lakini bomoabomoa hiyo haikumuacha salama Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule ‘Profesa J’.
Wamiliki wengi wa nyumba hizo hawajaanza kubomoa wenyewe kama ilivyo kwa wengine walioanza kufanya hivyo kwa hiari yao ili kuokoa baadhi ya mali kabla ya kubomolewa kwa nguvu na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).
Hali ya huzuni na simanzi imetawala kwenye maeneo ambako wananchi wamekumbwa na bomoabomoa hiyo, wengi wao wakilalamikia sheria ya mita 121.5 kila upande badala ya ile ya awali ya mita 60.
Mwananchi jana ilifika kwenye nyumba ya Profesa J na kukutana na alama ya X inayoonyesha kuwa nyumba hiyo (pichani) inatakiwa kuvunjwa.
Hivi karibuni, Tanroads ilitangaza kuwa muda wowote itaanza utekelezaji wa kubomoa nyumba zilizowekewa alama ya X katika barabara hiyo kupisha ujenzi wa barabara kubwa na kisasa.
Tayari Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeanza kukata umeme kwenye nyumba nyingi hivyo kuwafanya baadhi ya wenye nyumba kubomoa wenyewe kwa hiari na kufungasha mizigo.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Stop Over, Jumanne Juma alisema yapo majengo mengi ya kifahari yaliyokumbwa na bomoabomoa hiyo na kuwaweka wamiliki wake njiapanda.
Jumanne alisema kulikuwa na haja ya kuzungumza na wananchi kuwafafanulia sheria ya mita 121.5 zinazotumika sasa na kuona namna ya kuwalipa fidia badala ya kubomoa bila maelekezo yoyote.
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo walisema hali si shwari kwao kwani wengi wao wamejenga nyumba hizo kwa kujibana tofauti na inavyodhaniwa.
Mmiliki wa nyumba iliyopo Mbezi kwa Msuguri inayokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh150 milioni, Zuhura Jumanne alisema hali hiyo imewaathiri kisaikolojia kwani nyumba yake ipo nje ya mita 60.
“Sheria wanatunga wao, lakini ile iliyokuwa inajulikana ni mita 60. Presha inapanda na kushuka, kiukweli sijui hata tufanyaje maana tumechanganyikiwa,” alisema.
Zuhura ambaye alikuwa anazungumza kwa huzuni, alisema walianza kuijenga nyumba hiyo kidogo kidogo tangu mwaka 1995, wakijinyima matumizi mengine ili waje waishi vizuri na watoto.
“Kwa zaidi ya miaka 10 tumeijenga nyumba hii taratibu sana, nguvu yote inaisha kwa siku moja na sina pa kwenda na hawa watoto ambao pia wanasoma,” alisema.
Alisema nyumba yao ilisimama zaidi baada ya mume wake kupunguzwa kazini na kutumia kiinua mgongo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi.
Alisema siku aliyopata taarifa ya nyumba yake kuwa inabomolewa alipatwa na mshtuko kwa sababu alikuwa likizo jijini Mbeya.
“Hali haikuwa nzuri. Hata hivyo, tuliliwazana na kumshukuru Mungu kisha nikarudi na kuona ni kweli kuna X,” alisema.
Mmiliki huyo wa nyumba alieleza kuwa miaka yake yote nyumba hiyo imekuwa ikilipiwa kodi ya majengo na kwamba hata mwaka huu ameilipia Sh240,000 lakini sasa inabomolewa.
“Ninavyosema tumejenga kwa tabu naomba unielewe, tangu niolewe hadi umri huu sijawahi kuishi na mume wangu pamoja, siku zote yupo mikoani anatafuta maisha. Pamoja na ugumu huo, leo hii tutarudi kwenye maisha ya kupanga, nasikitika na naumia sana,” alisisitiza.
Alisema angepewa achague angeomba abaki na nyumba hiyo kwa sababu umri wake umeenda na hafikirii kama anaweza kusimamia ujenzi ukafikia kiwango ambacho tayari alishafikia.
“Hatuwezi kulalamika sana, ninachoomba ni huruma ya Rais atutazame watu wake sio kwamba tunazuia maendeleo, lakini hali hii tutaenda wapi? Umri wa kustaafu umefika tutaanzia wapi? Hatujui chochote na hatujasikia hata kama kuna fidia,” alisema.
Mwanafamilia mwingine wa nyumba ya kifahari katika eneo la Mbezi Luis, Laika Wilson alisema nyumba yao ilianza kujengwa mwaka 1995 ikiwa kwenye umbali wa mita 60 zinazotakiwa kisheria.
Wilson alisema wananchi wengi hawakuwahi kujua kama nyumba zao zitakuja kukumbwa na bomoabomoa jambo ambalo limewatetemesha.
“Walau leo mmekuja naweza kuzungumza, lakini tulipatwa na mshtuko mkubwa na hatua tuliyofikia hatujui nini kinaendelea, ni kama tumechanganyikiwa,” alisisitiza.
Alisema ni kweli kwamba, maendeleo ya nchi yanatakiwa kuwapo, lakini lazima wananchi wanaoharibiwa mali zao kwa sababu ya maendeleo hayo walipwe fidia.
“Thamani ya nyumba yetu inazidi Sh200 milioni, tumejenga kwa kujikongoja, lakini itabomolewa kwa siku moja. Ushauri wangu kwa Serikali wazungumze na sisi wananchi, watusikilize ndipo wabomoe, vinginevyo tunaonewa sana,” alisema.
Mmiliki huyo alisema mara zote amekuwa akijiuliza ni barabara gani inayojengwa ndani ya mita 121.5 na kuwaumiza wananchi, wengi wakiwa wa kipato cha chini hata hivyo, wanasubiri kuona matokeo zaidi.
Mnyika amwandikia Rais barua kuhusu bomoabomoa
Wakati hayo yakiendelea Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika amemwandikia barua Rais John Magufuli akimtaka kukutana naye ili kujadili masuala makuu matatu ikiwamo suala la bomoabomoa kwenye jimbo lake.
Suala jingine ni kuhusiana na uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini ambaye alitakiwa kusimamia mazungumzo yanayoendelea kuhusu mchanga wa madini ‘makinikia’ na Katiba Mpya.
Akizungumza juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Goba iliyopo Ubungo, Mnyika alisema anatarajia kukutana na Rais mara baada ya kumaliza ziara yake mkoani Tanga.
“Nimemwandikia barua Rais Magufuli ili nikutane naye ili tupate ufumbuzi kuhusu masuala haya,” alisema Mnyika.
Katika mkutano huo, Mnyika aliongozana na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob na madiwani wa kata mbalimbali na licha ya kuzungumzia shughuli za maendeleo, walieleza mambo ambayo yanahitaji kupewa ufumbuzi kwa manufaa makubwa ya Taifa.
Alisema hana pingamizi na suala la bomoabomoa lakini hakubaliani na vipimo ambavyo Tanroads wanatumia na kwamba imesababisha watu kupoteza mali zao na kuongeza migogoro.
“Mita 121.5 ukijumlisha kila upande ni sawa na viwanja viwili na nusu vya mpira, hakuna barabara kama hiyo Tanzania nzima,” alisema.
Alisema mbali na kuzungumza na Magufuli, amepeleka muswada wa Sheria kwa Katibu wa bunge ili kuhimiza marekebisho ya Sheria ili kuepusha migogoro na wananchi.