KAMANDA WA POLISI MKOA WA TANGA, BENEDICT WAKULYAMBA.
MAKONDAKTA wawili wa mabasi wamekufa kwa kugongwa na moja kati ya mabasi yao wakati wakigombea abiria kituoni.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, makondakta hao walikumbwa na umauti eneo la Mkwaja wilayani Pangani jana majira ya saa moja asubuhi wakati wakigombea abiria waliokuwa wanaelekea Tanga mjini.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Shehe Mpendeza aliyekuwa kondakta wa basi la Kampuni ya Moa Trans lenye namba za usajili T347 BCZ na Bashir Kibai wa basi la Kampuni ya Tawfiq lenye namba T365 AQU.
Kamanda Wakulyamba, akieleza zaidi kuhusu tukio hilo, alisema basi la Moa lilikuwa linafanya safari zake kati ya Tanga na Kipumbwi na Tawfiq lilitokea Mkwaja kwenda Tanga na yalikutana kijiji cha Mwera wilayani humo ambako kulikuwa na abiria wa kwenda Tanga.
Alisema baada ya mabasi hayo kukutana hapo, makondakta hao walianza kugombea abiria na kondakta wa Moa alimwendea mwenzake kumnyang’anya abiria, jambo lililozua mapigano.
”Wakati wanakingiana njia ndipo dereva wa basi la Tawfiq alipopita mbele upande wa kushoto walikokuwa wakipigana, lakini ghafla akawagonga wote wawili na kupoteza maisha,” alisema.
Kamanda Wakyamba aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linawatafuta madereva wa mabasi hayo ambao walikimbia baada ya tukio hilo.
Alisema kuwa baada ya kupatikana, madereva hao watafikishwa mahakamani kutokana na kusababisha vifo hivyo.