Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad kimedai kuwa hatua ya ofisi ya Spika kumtambua Magdalena Sakaya kama kaimu katibu mkuu wa chama hicho ni maelekezo ya ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Agosti 4, ofisi ya Spika ilimwandikia barua Maalim Seif ikimwarifu kwamba ina barua ya mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba iliyoandikwa Machi 20 ikimtambua Sakaya kama kaimu katibu mkuu.
Barua hiyo ya Profesa Lipumba ililiarifu Bunge kuwa Maalim Seif ameshindwa kutekeleza majukumu yake kama katibu mkuu na kwa mujibu wa katiba ya CUF na kwamba, majukumu ya katibu mkuu yatatekelezwa na Sakaya kuanzia tarehe hiyo. Kutokana na hilo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alimjibu Maalim Seif kwamba anashindwa kuifanyia uamuzi barua yake kutokana taarifa alizozipokea awali.
Wiki iliyopita, Maalim Seif alimwandikia barua Spika na nakala yake kwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Katika barua hiyo, Maalim Seif alitangaza kuwafukuza uanachama wabunge wawili ambao ni Sakaya (Kaliua – Tabora) na Maftaha Nachuma (Mtwara Mjini) kwa makosa ya kukihujumu chama hicho.
Hatua hiyo ya Maalim Seif ilikuja siku chache baada ya Baraza Kuu la Uongozi la CUF upande wa Profesa Lipumba kuwavua uanachama wabunge wanane. Wabunge waliovuliwa uanachama ni Halima Ali Mohamed, Khadija Salum Ally, Salma Mohamed Mwasa, Miza Bakari Haji, Raisa AbdMussa, Riziki Mngwali, Saumu Heri Sakala na Severina Mwijage.
Akizungumza na wanahabari jana, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF upande wa Maalim Seif, Joran Bashange alidai kuwa kilichosemwa na Spika hivi karibuni si uamuzi wake bali ni msajili ndiye aliyemwandikia barua akimweleza kumtambua Profesa Lipumba
“Msajili huyuhuyu ndiye kaandika barua kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hadi katika taasisi za haki na binadamu na utawala wa sheria ikieleza kwamba anayetambulika ni Profesa Lipumba na kaimu katibu mkuu ni Sakaya,” alisema Bashange.
Alifafanua kwamba kwa mujibu wa katiba ya CUF hakuna kipengele kinachoeleza nafasi ya kaimu katibu mkuu na huo ni mwendelezo wa hujumu zinazofanywa dhidi ya chama hicho kwa lengo la kukiua.
Bashange aliendelea kudai kuwa msajili alipeleka barua za kumtambua Profesa Lipumba na Sakaya bila kunukuu vifungu vya katiba ya chama hicho.
Awali, Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, Mbarala Maharagande alisema wabunge waliovuliwa uanachama na kupoteza sifa ya kuwa wako imara na marekebisho waliyotakiwa kuyafanyia kazi na Mahakama Kuu yamekamilika.
Mbali na hilo, Maharagande alidai kwamba Profesa Lipumba bado anaendelea kukihujumu chama hicho na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa kuwa ni miongoni wa watu waliofanikisha ushindi wa nafasi ya unaibu meya wa Mtwara ulioangukia mikononi mwa CCM.
Mwananchi: