Ngoma avishwa 'mabomu' Yanga

LICHA ya Simba kuonekana imejiimarisha zaidi katika safu ya ushambuliaji, kocha wa Yanga, George Lwandamina, anaamini straika wake, Donald Ngoma, ataendelea 'kuzilipua' timu za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kutupia mabao pindi itakapoanza hapo Agosti 26, mwaka huu.

Lwandamina ambaye alirithi mikoba ya Mholanzi Hans van der Pluijm, amesema bado hajaona mshambuliaji anayeweza kumfunika Ngoma, ambaye msimu uliopita alisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.

Kocha huyo alisema kuwa Ngoma ana faida ya kuizoea Ligi Kuu ya Bara tofauti na washambuliaji wa timu nyingine waliosajiliwa.

"Nina imani na safu yangu ya ushambuliaji, najua itafanya kazi yake vizuri katika ligi ya Tanzania na mashindano mengine ya kimataifa ambayo watashiriki mwakani," alisema Lwandamina.

Aliongeza kuwa mechi za kirafiki ambazo wanaendelea kucheza zitawasaidia kujiimarisha kabla ya kuanza kwa ligi kuu ambayo inashirikisha klabu 16 kutoka mikoa mbalimbali.

"Sasa ninaifahamu ligi, ninazijua timu tofauti na pale nilipojiunga msimu uliopita, ninaamini mambo yatakwenda vizuri kwa sababu changamoto na ushindani ninauelewa," aliongeza kocha huyo wa zamani wa Zesco.

Wakati huo huo, Yanga inatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Ruvu Shooting itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, alisema kuwa mechi hiyo itazisaidia timu zote kujiimarisha, lakini akitamba kikosi chake kina uwezo wa kuwafunga mabingwa hao wa Bara.

Yanga itaanza kutetea ubingwa wanaoushikilia kwa kuikaribisha Lipuli FC ya Iringa.