F Tembo wapiga kambi kata ya Mkoka, wamjeruhi mtu na kula mzao mashambani | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Tembo wapiga kambi kata ya Mkoka, wamjeruhi mtu na kula mzao mashambani

Na. Ahmad Mmow, Nachingwea.
WANANCHI wanaoishi kwenye vijiji vilivyopo katika kata ya Mkoka wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi, wapo kwenye taharuki kutokana na ujio wa tembo kwenye kata hiyo.

Taarifa toka idara ya maliasili ya halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, imeeleza kuwa  tembo hao wanaoendelea kuvinjari kwenye baadhi ya vijiji vilivyopo kwenye kata hiyo, licha ya kuharibu mazao kwenye baadhi ya mashamba,lakini pia wamejeruhi mtu mmoja katika kijiji cha Narungombe.

Akieleza matukio hayo, ofisa wanyama pori wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kwaniaba ya ofisa maliasili na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri, Benjamin John, alisema tembo hao wanaokadiriwa kuwa kumi walikwenda katika kijiji cha Narungombe tarehe 21 mwezi huu, ambapo walimjeruhi mtu mmoja anaetambulika kwa jina la Said Mbujeje aliyekuwa shambani mwake akiwa anavuna mbaazi.


"Nikweli tukio hilo limetokea nasisi tulikwenda huko lakini hatukuwakuta, hata hivyo tumeambiwa  jana (juzi)usiku wameonekana katika kijiji cha Rweje. Leo (jana) tumeambiwa wapo katika kijiji cha Mkoka katika kitongoji cha Mpuju wanakunywa maji kwenye bwawa, tunataka kwenda huko, "alisema Benjamin.

Ofisa huyo alisema wajibu wao ni kwenda kuwafukuza kutoka kwenye maeneo yaliyo karibu na makazi ya watu na kuwarejesha hifadhini. Mbali na kueleza hayo, ofisa huyo alitoa wito kwa wakulima kuweka mizinga ya nyuki na kupanda pilipili kuzunguka mashamba yao. Akiweka wazi kuwa tembo hawapendi pilipili na nyuki. "Katika kipindi hiki cha Kiangazi tembo huwa wanavuka toka nchini Msumbiji na kuja huku. Wanapitia Mangaka, Matekwe,hifadhi ya Msanjesi, msitu wa Lionja, Lipuyu.

Hivyo vijiji vya wilaya ya Nachingwea, ndipo wanaingia wilaya ya Liwale katika kijiji cha Mirui na kuvuka mto Mbwemkuru na kuingia tena katika wilaya ya Nachingwea katika vijiji vya Namapwia, Kipara hadi kwenye kata hiyo ya Mkoka, "alifafanua Benjamin.

Kwa upande wake Said Mbujeje ambae amelazwa katika hosipitali ya wilaya ya Nachingwea, alisema alikutana na dhahama (mkasa) hiyo juzi jioni majira ya saa 11 jioni, akiwa shambani mwake akiwa anavuna mbaazi." Nilisitushwa na vilio vya watoto wao, nilijaribu kukimbia lakini nilianguka. Tembo mmoja aliniwahi, akanishika na kunirushia porini. nilipoteza fahamu toka saa 11 jioni nililala kwenye eneo hilo hadi saa 1 jioni.

 "alisema Mbujeje. Majeruhi huyo ambae anaendelea na matibabu, ambae pia aliwasifu na kuwashukuru wauguzi, waganga na madaktari wa hosipitali hiyo kwa kumpa huduma zinazotolewa kwake na wagonjwa wengine, alisema baada ya kumtipia porini walikula mbaazi, migomba na kuvunja mikorosho kwenye shamba lake.

"Baada ya kutoka shambani kwangu walikwenda kijijini (Narungombe) walikaa masaa manne pale   kijijini, wakatimkia Nandile. Leo nasikia wapo Mkoka eneo la Mpuju wanakunywa maji bwawani, "aliongeza kusema Mbujeje. Nae kaimu mganga wa hosipitali hiyo, Dkt Faraja Peter alisema Mbujeje anaendelea kupata matibabu na hali yake inaendelea vizuri." Alipata maumivu kwenye mbavu na michubuko, hata hivyo kesho (leo) tunatarajia atapimwa kwa kutumia eksirei (X-ray) tulimpokea jana, anaendelea vema tunashukuru, "alisema Dkt Faraja ambae muda wote alionesha kujali kazi yake na kumtanguliza Mungu katika mazungumzo yake .

Serikali ipo kwenye jitihada kubwa ya kupambana na ujangili ambao ulitishia kuwafuta wanyama hao. Sasa uhenda hali hiyo ni matokeo chanya ya juhudi za serikali. Kwamba hivi sasa wamezaliana na kuongezeka na wapo salama dhidi ya ujangili.