Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoani humo kuwasaka watu wote waliohusika katika jaribio la mauaji ya watu wanne ambao walipigwa na kuwachoma moto katika kijiji cha Mwanabondo, Wilayani Uyui Mkoani humo kwa tuhuma za ushirikina.
Mwanri amesema kuwa vitendo vya wananchi kuendelea kujichukulia sheria mikono havivumiliki na havikubaliki hata kidogo kwa kuwa vyombo vya sheria vipo ambavyo vinaweza kutekeleza majukumu yake.
Mkuu huyo wa Mkoa ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa amesema licha ya tukio hilo kutokea lakini sio la kwanza hivyo vyombo vya usalama lazima vihakikishe vinawatia nguvuni watu wanaotekeleza matukio hayo.
Wakiongea wakiwa Hospitali Mkoani humo baadhi ya wahanga wa Tukio hilo wamesimulia jinsi walivyotaka kuuawa na watu hao wasiojulikana ambao walitokomea mara baada ya kushindwa kutekeleza azma yao.