F Mkondya aaga Dar akimkumbuka Tundu Lissu | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mkondya aaga Dar akimkumbuka Tundu Lissu

ALIYEKUWA Kaimu Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, amesema analiacha Jiji likiwa shwari na changamoto iliyopo ni wanasiasa kutokutii sheria.

Mkondya aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza kuzungumza na waandishi wa habari. Aliulizwa swali kuhusu changamoto anazomwachia Kamanda mpya wa kanda hiyo,  Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Lazaro Mambosasa.

“Ukiwa mwanasiasa si kinga ya wewe kutotii taratibu za nchi, ni lazima ufuate taratibu za nchi na sheria ziko pale pale. Kwa Dar es Salaam changamoto hizi ni nyingi mno,” alisema.

“Kwanza niseme kwamba Dar es Salaam naiacha ikiwa shwari. Kuna uhalifu wa matukio machache machache ambayo yanatokea hapa na pale lakini kwa ujumla Dar es Salaam ni shwari.”

Alisema anaamini Kamanda Mambosasa atapambana na changamoto hizo kwa kuwa ni kamanda shupavu mwenye weledi mkubwa na uelewa.

Wakati huo huo, Kamanda Mkondya  alisema katika eneo la Tabata Chang’ombe majira ya saa 2:30 usiku askari wa kikosi kazi maalum wakiwa katika doria maeneo hayo walipata taarifa kuwa kuna kikundi cha watu kimepanga kufanya tukio la kihalifu.

Alisema askari walifuatilia na wahalifu hao baada ya kuwaona askari walikurupuka na kukimbia kusikojulikana.

“Baada ya askari kufanya upekuzi katika eneo hilo ndipo walifanikiwa kukamata bastola moja aina ya Browning ikiwa na risasi nne kwenye magazine namba zake zikiwa zimefutwa,” alisema

Aidha, alisema katika tukio lingine katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere wakiwa katika doria, walimkamata jambazi aliyefahamika kwa jina la Khalid Likwaulo akiwa na bunduki aina ya Shotgun iliyokatwa kitako ikiwa na risasi mbili ndani ya magazine.

“Jambazi huyo alikamatwa akiwa na pikipiki yenye namba za usajili MC.161 AXF aina ya Boxer rangi nyeusi. Aliamua kuiacha na kukimbia baada ya kuwaona askari eneo hilo na alipokaguliwa alikutwa na silaha hiyo,” alisema Mkondya.

Alisema uchunguzi unaendelea ili kubaini kundi lake analoshirikiana nalo kufanya uhalifu na kujua siku hiyo walikuwa wamejipanga kufanya wapi uhalifu.

Aidha, alisema katika oparesheni maalum ambayo imefanyika Agosti 18 hadi Agosti 24 mwaka huu,  wamefanikiwa kuwakamata wahalifu 130 kwa makosa mbalimbali ya kihalifu.