F TRA kufuatilia mabasi yasiyochukua risiti za EFD | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

TRA kufuatilia mabasi yasiyochukua risiti za EFD

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Rukwa, imefanya msako maalumu wa kukagua mabasi ya abiria na magari ya mizigo ambayo hayajalipiwa stika za taasisi hiyo na kuchunguza iwapo wanachukua risiti kwa kutumia Mashine za Kielektroniki (EFD) wanapojaza mafuta katika vituo vinavyouza nishati hiyo.

Msako huo ulianza saa 11:00 alfajiri katika stendi kuu ya mabasi iliyopo mjini Sumbawanga, walianza kuyakagua yanayotoka mjini na kuelekea katika wilaya za mkoa huo na baadaye mabasi yanayokwenda mikoani.

Akizungumza wakati akiongoza msako huo jana, Meneja Msaidizi Idara ya Ukaguzi wa TRA Mkoa wa Rukwa, Amina Shamdas alisema mamlaka hiyo inashirikiana na Kampuni ya Yono Auction Mart.

Shamdas alisema mamlaka hiyo ilibaini wafanyabiashara wa usafirishaji wamekuwa hawadai risiti zinazotolewa na mashine za EFD wanaponunua mafuta na kwamba, magari mengi yana stika za kughushi za kulipia mapato ndiyo sababu waliamua kufanya msako huo.

Alisema kufuatia msako huo, anaamini wafanyabiashara hao watabadilika na kuanza kufuata sheria ili kuepukana na mkono wa sheria vinginevyo watajikuta katika wakati mgumu wanapofanya biashara zao.

Aliongeza kuwa umefika wakati sasa kila mwananchi aone fahari kulipa kodi, kwani kwa kufanya hivyo atakuwa ametimiza wajibu wake kwa Taifa na hatopata usumbufu wowote kwenye shughuli zake.

Naye Mwakilishi wa Yono mjini Sumbawanga, David Phillipo alisema wamekuwa wakikutana na changamoto kubwa kutoka kwa wafanyabiashara hao, baadhi wamekuwa wakaidi katika kutii sheria.

Phillipo alisema kwa kuwa wamejipanga vizuri kwa kushirikiana na TRA, watahakikisha hakuna mapato yatakayopotea kwani lazima Serikali ikusanye kikamilifu ili kuwahudumia wananchi wake.

Alisema wafanyabiashara wanatakiwa kushirikiana na Serikali kwa kulipa kodi zinazotakiwa vinginevyo watakuwa wanajiingiza kwenye matatizo, watakapokamatwa lazima wafikishwe mahakamani.    

Mwananchi: