SERIKALI imesema jumla ya walimu 2,939 sawa na asilimia 19.5 walioomba kujiunga na mafunzo ya ualimu ngazi ya astashahada na stashahada kwa mwaka wa masomo 2017/18, wamebainika kutokuwa na sifa zinazotakiwa kujiunga na mafunzo hayo.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Dk. Leornard Akwilapo, alipozungumza na vyombo vya habari.
Alisema kati ya walimu 15,091 waliomba kujiunga na mafunzo hayo wanawake wakiwa 6,051 na wanaume 9,040 waombaji 12,152 sawa na asilimia 80.5 walikuwa na sifa stahiki za kujiunga na programu za uwalimu walizoziomba.
Alifafanua nafasi za mafunzo ya ualimu katika vyuo vya ualimu vya serikali zilizotangazwa zilikuwa ni 5,375 kwa programu ya astashahada ya elimu ya ualimu na 3,731 za stashahada mbalimbali za ualimu.
“Jumla ya nafasi za udahili kwa mafunzo ya ualimu kwa mwaka wa masomo 2017/2018 zilikuwa 9,106 katika vyuo 30, ambapo kati ya hivyo, vyuo 23 vinatoa mafunzo ya ualimu katika ngazi ya astashahada huku vyuo 16 vikitoa mafunzo hayo katika ngazi ya stashahada,” alisema.
Kadhalika, alisema uchaguzi wa waombaji ulizingatia vigezo vya jumla ambavyo ni ufaulu wa daraja la I hadi III kwa kidato cha nne kwa waombaji wa astashahada na kidato cha sita kwa waombaji wa stashahada.
Dk. Akwilapo alisema waombaji wa Astashahada waliofaulu masomo ya Sayansi katika kidato cha nne walipewa kipaumbele.
Alisema ufaulu wa juu wa waombaji waliochaguliwa kwa kozi ya Astashahada ni daraja la I, alama 14 na kwa Stashahada ni daraja la I, alama sita.
“Ufaulu wa chini kwa waombaji wa kozi ya Astashahada ni daraja III, alama 25 na kwa Stashahada ni daraja la III, alama 17,” alisema.
Katibu Mkuu huyo alisema jumla ya waombaji 7,578 wamechaguliwa na kupangiwa vituo kwa ajili ya mafunzo ya ualimu katika ngazi hizo katika vyuo vya serikali vya ualimu.
Alisema nafasi zilizobaki wazi katika vyuo vya ualimu vya serikali bila kujazwa ni 1,528 na majina yaliyochaguliwa yanapatikana katika tovuti ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Aidha, alisema vyuo vya ualimu vinatarajia kufunguliwa Septemba 25, mwaka huu na wote waliochaguliwa watajulishwa na vyuo husika kuhusu utaratibu wa kufika na kuanza masomo.
Kwa mujibu wa Dk. Akwilapo, kwa kuzingatia kuwa bado kuna vyuo vyenye sifa zilizo wazi NACTE ilitoa fursa ya kuwasilisha maombi kwenye programu za Astashahada na Stashahada katika fani mbalimbali nchini kuanzia Septemba 18 hadi Oktoba mosi mwaka huu.