F Dawa za kulevya zakamatwa | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Dawa za kulevya zakamatwa

Mwanza. Maofisa wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) wakishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama usiku wa kuamkia juzi walikamata zaidi ya kilo 100 za mihadarati aina ya heroin zilizokuwa zikisafirishwa kwenye jahazi kutoka Unguja kwenda Dar es Salaam.

Maofisa hao wa nchini wakishirikiana na vyombo vingine vya kimataifa walilitilia shaka na kuamua kulizuia jahazi hilo lililokuwa na raia kumi wa Iran na Wazanzibari wawili.

Kamishna wa sheria wa DCEA, Edwin Kakolaki amesema baada ya upekuzi wa awali walifanikiwa kukamata paketi 104 za dawa wanazoshuku kuwa ni heroin ambazo watazipeleka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa vipimo.

“Tunaendelea na ukaguzi wa jahazi na sasa tumepeleka mbwa kusaidia kazi hiyo,” alisema Kakolaki.

Hadi jana jioni maofisa wa DCEA walikuwa wakifanya upekuzi kwa kusaidiwa na mbwa wanusaji kuona kama kuna mizigo zaidi.

Habari zaidi zinasema baada ya kuona wamezungukwa, raia hao wa Iran walijaribu kubadili mwelekeo, lakini walizidiwa nguvu na kuanza kutupa baadhi ya mizigo kwenye maji ya Bahari ya Hindi.

Kamishna Mkuu wa DCEA, Rodgers Siyanga amesema kiwango hicho cha dawa kingekuwa kikubwa zaidi isingekuwa kitendo cha watu hao kutupa kiasi kingine baharini.

“Nasema vyombo vya dola viko imara kupambana na usafirishaji wa dawa za kulevya na hatutaacha kuyadhibiti magenge na mitandao yao. Kwa hiyo mtu yeyote anayepanga kuingiza dawa za kulevya ni vema ajiulize mara mbili na aache, tutampata tu,” alisema Siyanga.

Meli iliyotumika katika operesheni hiyo ya usiku wa manane ilitumika pia kulivuta jahazi hilo na kulifikisha Bandari ya Dar es Salaam juzi saa nne usiku.

Ofisa mwingine aliyeshiriki operesheni hiyo alisema baada ya kukamatwa raia hao wa Iran walijitetea kuwa wao ni wavuvi. “Tulipowabana wakadai wanakwenda nchini Somalia kusaka chombo cha wenzao walichodai kutaarifiwa kimeharibika huko.”

Imeelezwa pia kuwa Wazanzibari wawili waliokutwa kwenye meli hiyo walijitetea kuwa wao walitumwa tu kupeleka chakula katika jahazi hilo.

Raisi John Magufuli aliwahi kusema Serikali yake haitakuwa na huruma na watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ambazo zimeharibu nguvu kazi ya Taifa kwa kiasi kikubwa.

Akiamuapisha Siyanga mwezi Aprili, Rais Magufuli alisema, ‘isingekuwa sheria imesema, yeye mwenyewe angekuwa mwenyekiti badala ya waziri mkuu’, huku akimtaka Kamishna Siyanga kufanya kazi bila woga.