Dar es Salaam. Deni la Taifa liliongezeka kwa asilimia 15 katika kipindi cha miezi 13 iliyopita hadi kufikia Julai, ripoti ya mapitio ya uchumi ya mwezi Agosti ya Benki Kuu (BoT) imeonyesha.
Tathmini ya mwenendo wa uchumi ya kila mwezi inayotolewa na BoT inaonyesha deni hilo lilifikia kiwango cha Sh53.3 trilioni kwa mwaka ulioishia mwezi Julai kutoka Sh46 trilioni kwa mwaka ulioishia Juni, 2016. Kiwango hicho pia kiliongezeka kutoka Sh52 trilioni za Juni.
Mwaka ulioishia Juni,2016 deni hilo liliongezeka kwa asilimia 20 kutoka Sh38.2 trilioni zilizorekodiwa Juni, 2015.
Kulingana na ripoti hiyo ya uchumi inayotolewa kila mwezi, deni hilo lilifika kiasi hicho kutokana na mikopo mipya kutoka vyanzo vya ndani na nje ukiwamo wa Dola 505 milioni za Marekani ambao Serikali iliuchukua kutoka Benki ya Credit Suisse ya Uswiwi mwezi Juni.
Uchambuzi wa deni hilo unaonyesha kiwango kikubwa cha fedha, asilimia 47.2 zilitoka kwenye mashirika ya kimataifa ambalo ni Dola 8,909 milioni wakati mikopo ya kibiashara ilikuwa Dola 1,510.2 milioni huku inayobaki na Dola 5,890 zikitokana na makubaliano na taasisi au nchi nyingine ambazo ni sawa na asilimia 43.6.
Deni hilo la Taifa ni sawa na nusu ya Pato la Taifa (GDP) ambalo linakadiriwa kuwa Sh103.7 trilioni kama ilivyokadiriwa kwenye ripoti ya mwaka ya BoT, 2016.
Hata hivyo, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) mwaka 2016 lilikadiria deni hilo kuwa asilimia 38 ya GDP kwa mwaka huu wa fedha.
Kiwango cha deni hilo katika kipindi cha mwaka 2001 hadi 2016 kinatajwa kuwa kilikuwa wastani wa asilimia 34.88 ya GDP. Hata hivyo, deni hilo lilipaa zaidi mwaka 2001 na kufika asilimia 50.2 ya GDP kabla ya kupungua na kufika kiwango cha chini, asilimia 21.50 mwaka 2008.
Shirika la Trading Economics linalofanya uchambuzi wa masuala ya uchumi hivi karibuni lilisema deni la nje la Tanzania liliongezeka hadi Dola 17.907 bilioni, Mei kutoka Dola 17.802 bilioni mwezi uliotangulia.
Kati ya mwaka 2011 mpaka Aprili 2017, shirika hilo lilisema deni la nje lilikuwa wastani wa Dola 13.06 bilioni, lakini Mei liliongezeka mpaka Dola 17.907 bilioni.
Kwa miaka saba mpaka sasa, deni hilo lilikuwa dogo zaidi Desemba 2011 likisomeka Dola 2.469 bilioni.
Katika ripoti yake ya Juni kuhusu ustahimilivu wa deni la Taifa (DSA), IMF ilisema Tanzania inaweza kufikia nakisi ya bajeti ya asilimia 4.5 ya GDP kwa miaka michache ijayo, hali itakayohitaji uchumi kujikinga dhidi ya hatari zozote zinazoambatana na ukuaji wa madeni.
Ripoti hiyo ya Juni, 2016 inaonyesha viashiria vitatu vya deni ikiwamo pato la Taifa, mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi na kodi viliongezeka kidogo katika kipindi cha muda wa kati kabla ya kushuka katika kipindi cha makadirio ya awali kuisha.
Marejesho ya deni kwa wastani wa kodi yaliongezeka kwa kipindi cha kati na kuwa katika kiwango cha juu kwenye kipindi cha muda wa mwisho wa makadirio hayo.
“Marejesho ya deni kwa wastani wa kodi yataongezeka katika kipindi cha mwaka 2020-23 kwa kiwango cha asilimia moja mpaka 30 cha kushuka kwa thamani ya fedha,” imesema IFM.
Kwa hali hiyo matokeo yanaonyesha hatari ya deni la Taifa ni ndogo kwa kuzingatia viashiria vyote vitatu vya kodi, pato la Taifa na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi.
Uchambuzi uliofanywa na BoT kuhusu ustahimilivu wa deni mwaka 2016 ulionyesha malipo ya deni hilo kwa kutumia kodi za ndani yamefikia asilimia 11.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20. Malipo ya deni kwa kutumia mauzo ya nje ni asilimia 7.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20.
BoT ilibainisha kiwango kikubwa cha deni kina muda mrefu wa marejesho wa wastani wa miaka 11.9. Hii ina maana ulipaji wa deni kwa kutumia bajeti una hatari ndogo ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2016 iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (Unctad), kiwango kikubwa cha deni la ndani ni stahimilivu na hakiwezi kuathiri ukuaji wa uchumi kwa miaka ya baadaye.
Source: Mwananchi