IGP Sirro apiga marufuku Mijadala kuhusu Lissu

Mkuu wa jeshi la polisi nchini, IGP Simon Sirro ametaka mjadala ufungwe mara moja kuhusu sakata la mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kupigwa risasi na watu wasiojulikana mnamo Septemba 7, 2017 akiwa mjini Dodoma.

IGP Sirro ametoa kauli hiyo leo akiwa ziarani jijini Mbeya wakati akizungumza na vikosi vya ulinzi na usalama ambapo amewaonya wanasiasa kuacha kuuendeleza mjadala wa jambo hilo na waliachie jeshi la polisi lifanye kazi yake.

Mbali na hilo IGP Sirro amewataka wananchi hususani wa mkoa wa Mbeya, kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutii sheria bila shuruti na kwamba, Jeshi la Polisi litahakikisha linawachukulia hatua kali za kisheria ili kukomesha tabia hiyo.

Aidha Sirro amedai kuwa takwimu za uingizwaji na utumiaji wa dawa za kulevya imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kufanyika kwa operesheni za mara kwa mara zinazofanywa na Jeshi hilo la polisi.