Mkutano wa ALAT waanza Dar

 Mkutano wa 33 wa Jumuiya ya Tawala na Serikali za Mitaa ALAT umeanza leo jijini Dar es Salaam huku mwenyeji ambaye ni  Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita amesema kupitia mkutano huo wataiomba serikali  ili iweze kurudisha vyanzo vya mapato vilivyokuwa katika halmashauri.


Meya Mwita alizungumza kauli hiyo jijini hapa jana wakati akitoa salamu za kuwakaribisha wajumbe wa mkutano wa ALAT unaofanyika jijini hapa badala ya Mkoani Meya.

Meya Mwita alisema vyanzo vya mapato ambavyo vilikuwa vikisimamiwa na halmashauri ,Majiji viliwezesha kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali hususani huduma za kijamii.

Alifafanua kuwa vyanzo hivyo kuwa ni matangazo ya barabarani sambamba na kodi za majego ambapo kwa kiasi kikubwa zilikuwa zikiiletea halmashauri fedha ambazo zilitumika kuboresha huduma za afya, elimu na barabara.

Aliongeza kuwa kwakuzingatia ustawi wa halmashauri hizo ,mkutano huo utajadili na kumfikishia Rais Dk. John Magufuli ili fedha hizo zirudi kwa ajili ya maendeleo hususani Vijijini, Kata na Majiji.

“ Hali ya Halmashauri nyingi kifedha sio nzuri, na hii ni baada ya vyanzo hivi vya mapato ambavyo tulikuwa tunategemea kuchukuliwa, katika hali yoyote hakuna halmashauri ambayo itakuwa na fedha” alisema Meya Miwta.

Meya Mwita alitolea mfano halmashauri ya Ilala iliyopo katika jiji la Dar es Salaam kuwa kupitia vyanzo hivyo ilikuwa ikikusanya zaidi ya bilioni 68 ambazo zilikuwa msaada mkubwa katika kutoa huduma za kijamii ndani ya halmashauri hiyo.